RUFAA iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Ubungo, Hawa Ng’humbi (CCM), kupinga ushindi wa Mbunge wa jimbo hilo, John Mnyika, inasikilizwa leo.
Hawa, anapinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyompa ushindi Mnyika, katika kesi ya uchaguzi dhidi yake.
Rufaa hiyo, inatarajiwa kusikilizwa leo mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Salum Massati, Catherine Oriyo na Nathalia Kimaro.
Rufaa hiyo, ilifunguliwa Oktoba 25, 2012 na aliyekuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Ubungo mwaka 2010, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ng’humbi, aliyekuwa mlalamikaji katika kesi ya msingi.
Mahakama Kuu katika hukumu yake, iliyotolewa na Jaji Upendo Msuya Mei 24, 2012, ilitupilia mbali madai ya Ng’humbi ikisema alishindwa kuyathibitisha na badala yake, ikamthibitisha rasmi Mnyika kuwa mbunge halali wa jimbo hilo.
Hata hivyo, Ng’humbi hakukubaliana na hukumu hiyo na kuamua kukata rufaa Mahakama ya Rufaa Tanzania, akiiomba itengue hukumu hiyo ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Ng’humbi anayewakilishwa na Wakili Issa Maige, katika rufaa yake ameorodhesha hoja 10 za kupinga hukumu hiyo, akidokeza kile anachokiona kuwa ni udhaifu katika hukumu hiyo.
Ng’humbi anadai, Jaji Msuya alikosea katika kutafsiri sheria na kupima ushahidi wa pande zote, alikosea kisheria na kiukweli kwa kusema makosa yaliyobainika katika ujumlishaji na kuhesabu kura na kusababisha kuwapo kwa kura 14,854, zisizohesabiwa hayakuathiri matokeo ya uchaguzi.
Anadai aliweza kuthibitisha kuwapo kwa makosa katika mchakato wa uchaguzi, yaliyosababisha kuwapo kwa kura 14, 854 zisizohesabiwa, hivyo jaji alikosea kisheria na kiukweli kwa kutokuhamishia kwa mdaiwa, jukumu la kuelezea sababu za kuwapo kwa dosari hizo.
“Jaji alijipotosha kwa kumshutumu mrufani kwa kutokubainisha kuwa makosa ya msingi yaliyobainika katika kujumlisha na kuhesabu kura yalikuwa ya nia mbaya.
“Jaji alikosea kisheria na kiukweli kusema kura 14,854, ambazo hazikuhesabiwa zilitokana na makosa ya kibinadamu, bila kuwepo na ushahidi kuhusu hilo katika kumbukumbu za mahakama,” alidai mrufani katika hoja hizo.
Katika hoja nyingine, Ng’humbi anadai jaji alikosea kisheria kusema kuwa hazikutumika kompyuta ambazo hazikuwa zimeidhinishwa na mamlaka husika wakati wa kujumlisha kura.
Ng’humbi anaendelea kudai alishindwa kujielekeza sawa katika tofauti kati ya jukumu la kisheria kuthibitisha madai na wajibu wa kukanusha ushahidi.
Anadai matokeo yake, Jaji Msuya alihitimisha kimakosa katika masuala yaliyohusika katika kesi hiyo.
Source: Mtanzania
No comments:
Post a Comment