Monday, December 31, 2012

Padri aliyepigwa Risasi Zanzibar Azidi kufichua Mazito

Padri Ambrose Mkenda akiwa Hosptali ya Muhimbili
Padri  wa Kanisa Katoliki aliyepigwa risasi na watu wasiojulikana Zanzibar, Ambrose Mkenda, amesema kuna genge la watu ambalo limekuwa likifanya vitendo vya hujuma dhidi  viongozi wa dini na raia wasiokuwa na hatia Zanzibar.

Padri Mkenda ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mpendae,  alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, aliyefika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jana kumjulia hali baada ya kupigwa risasi Desemba 25, mwaka huu.

Padri Mkenda alisema yapo mazingira ya wazi juu ya kuwapo kwa kikundi cha watu ambao wamekuwa wakiwatumia vijana  wasio na ajira kufanya vitendo vya hujuma dhidi ya raia wasio na hatia na kusababisha baadhi ya watu kupata ulemavu wa maisha.


Alisema vitendo hivyo vimekuwa vikifanyika kwa lengo la kuwavunja moyo ili wapunguze harakati zao za kuhubiri amani miongoni mwa jamii visiwani Zanzibar.

Alisema amekuwa akiishi Zanzibar tangu mwaka 1995 akifanya kazi zake za kiroho katika mazingira ya amani, lakini katika miaka ya karibuni misingi ya amani na umoja wa kitaifa imeanza kuzoroteshwa na baadhi ya watu bila ya kuzingatia athari kwa Taifa.

“Nimekuwapo Zanzibar tangu mwaka 1995 nikifanya kazi ya mahubiri...kama kazi yangu inafahamika, sasa mkasa huu utasemaje kuwa una uhusiano na ujambazi wa kutaka mali?,” alihoji Padri Mkenda.

Padri Mtenda alisema serikali lazima ichukue hatua dhidi ya vikundi ambavyo vimekuwa vikichezea amani na umoja wa kitafa kwa maslahi ya watu binafsi na kuathiri maendeleo ya wananchi wake.

Hata hivyo, Padri Mkenda aliwashukuru viongozi mbalimbali wa serikali waliofika kumjulia hali pamoja na hatua walizoahidi kuchukuliwa na serikali katika kupambamna na vitendo hivyo vya uhalifu dhidi ya raia na mali zao.

Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, jana naye alifika Muhimbili kumjulia hali kiongozi huyo wa kiroho.

Padri Mkenda alisema jamii inapaswa kuzingatia amani na upendo katika maisha ya kila siku ili kuzalisha kizazi bora kitakachoheshimu haki na maadili ya binadamu.

Kwa upande wake, Balozi Seif alisema viongozi wa dini ni watu muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu na kutaka mchango wao kuheshimiwa na wananchi katika kuimarisha amani na umoja wa kitaifa.

Balozi Seif alisema jamii imekuwa ikiishi kwa amani na utulivu kutokana na mchango mkubwa wa viongozi wa dini ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kulinda misingi ya umoja wa kitaifa kwa kuwahimiza waumini wao kutenda mambo mema.

“Suala la amani liwe ya taifa au jamii husika, linamuhusu kila mtu na ushahidi wa hayo unapatikana katika vitabu vyote vya dini ambavyo vimekuwa vikihubiri amani kila wakati,” alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Viongozi wengine ambao wameshamtembea Muhimbili Padri Mkenda ni Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed.

Tukio la kupigwa risasi kiongozi huyo lilitanguliwa na tukio la kumwagiwa tindikali Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga, pamoja na wamiliki watano wa maduka ya pombe ambapo mmoja alipoteza maisha.

Aidha, makanisa 25 pamoja na baa 12 zilichomwa moto na watu wasiojulikana kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2012. Hata hivyo,  hakuna  mtu aliyekamatwa kuhusiana na matukio hayo.

Padri Mkenda alipigwa risasi shingoni saa Desemba 25, mwaka huu 1:45 usiku wakati akisubiri kufunguliwa mlango (geti) nyumbani kwake  eneo la Tomondo alipokuwa akitoka kumwangalia mgonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja.

Wakati huo huo, Jeshi la Polisi Zanzibar linawashikilia watu wawili kwa kuwahusisha na tukio la kupigwa risasi kwa Padri Mkenda.

Ofisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mohamed Mhina, jana alithibitisha kukamatwa kwa watu hao usiku wa kuamkia jana mjini Zanzibar katika msako uliofanywa na makachero wa polisi kutoka Makamo Makuu ya Jeshi hilo jijini Dar es Salam kwa kusaidiana na polisi wa Zanzibar.

Hata hivyo, Mhina alikataa kutaja majina yao kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kutavuruga uchunguzi.

Mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, alituma timu ya makachero kwenda Zanzibar kusaidiana na polisi wa huko kufanya uchunguzi huo.



Source: IPP Media

No comments: