Rais Jakaya Kikwete |
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ameonyesha kushangazwa na kasi ya ongezeko la watu nchini Tanzania ambalo limefikia asilimia 2.6 kwa mwaka.
Rais Kikwete alionyesha kushangazwa huko wakati alipokuwa akitangaza matokeo ya sensa ya watu na makazi mjini Dar es Salaam ambapo matokeo yanaonyesha kuwa Tanzania ina watu 44,929,002 ambapo Tanzania Bara kuna watu 43,625,434 na Zanzibar kuna watu 1,303,568.
"Kama kasi ya ongezeko la watu la asilimia 2.6 halitapungua ifikapo mwaka 2016 nchi yetu itakuwa na watu milioni 51.6. Inawezekana idadi hiyo ikaonekana kuwa siyo tatizo la kuumiza kichwa kwa nchi kubwa kama yetu, lakini ni mzigo mkubwa kwa taifa, jamii na uchumi kuwahudumia" Alisema Rais Kikwete.
"Inabidi pawepo na mikakati madhubuti na ionekane katika mipango ya maendeleo kuanzia sasa jinsi ya kuhudumia watu hao 51.6 na zaidi ya hao miaka inayofuata. Kwa familia, lazima tutambue umuhimu wa kupanga uzazi, vinginevyo hali ya maisha itashuka sana. Kwa ujumla hatuna budi kufanya kazi kwa bidii zaidi na nguvu zaidi."
Takwimu zinaonyesha kuwa katika Sensa ya tatu ya mwaka 2002 idadi ya watu Tanzania ilikuwa ni milioni 34.4 ambapo kwa matokeo ya sasa ya idadi ya watu 44,929,002 ni sawa na ongezeko la watu milioni 10.5 sawa na asilimia 2.6 kwa mwaka.
Sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 ambapo Tanzania ilikuwa na watu 12,313,054. Tanzania Bara ilikuwa na watu 11,958,654 na Zanzibar watu 354,400. Kwa maana hiyo, katika miaka 45 tangu Sensa ya kwanza na hii, Watanzania wameongezeka kwa watu milioni 33.
No comments:
Post a Comment