MATOKEO mabaya ya mtihani wa kidato cha nne yamezidi kuibua mapya, baada ya wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini kusema mitihani ilitungwa kwa mfumo tofauti na uliozoeleka miaka yote, huku tume iliyounndwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ikipondwa na baadhi ya watu.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema kwamba maswali waliyoulizwa watahiniwa yalikuwa ya kujieleza tofauti na miaka ya nyuma, ambapo mfumo uliotumika uliwataka watahiniwa kutaja vitu tu bila ya kulazimika kuvielezea kwa undani.
Kauli yake iliungwa mkono na Mkuu wa Taaluma katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Marian, Florence Mapunda ambaye alisema kuwa mtihani wa mwaka jana ulitaka zaidi watoto kujieleza tofauti na miaka ya nyuma wakati wanafunzi walipokuwa wanakariri.
Hata hivyo, Msemaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), John Nchimbi alisema mfumo wa mtihani haukubadilika kwa namna yoyote na kuwa upo kama ule wa miaka yote.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, kwa upande wake alisema madai yanayotolewa hayana msingi, huku akihoji kwa nini yasitoke tangu mitihani ilipokuwa ikifanyika na badala yake yanatoka baada ya kutangazwa kwa matokeo.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na asilimia 60.6 wamepata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia 26.02 wamepata daraja la nne.
Kutokana na matokeo hayo, Waziri Mkuu Pinda, juzi alitangaza kuunda tume ya kuchunguza chanzo cha matokeo hayo kuwa mabaya, hatua ambayo hata hivyo imekosolewa na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Tume hiyo inayoundwa na wajumbe kutoka Taasisi za Elimu, Chama cha Waalimu, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii na Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa) inatarajiwa kuanza kazi wiki hii.
Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alisema kuunda tume ni kupoteza muda kwa sababu matatizo na changamoto zote ndani ya sekta hiyo yanajulikana, huku mwenzake, Profesa Chriss Maina pia wa UDSM akisema kuunda tume hakutaisaidia kwa kuwa Serikali inaidharau sekta ya elimu.
“Tatizo ni kutowekeza kikamilifu katika sekta ya elimu, imekuwa na matumizi makubwa katika mambo yasiyokuwa ya lazima,”alisema Profesa Mpangala.
Alisema matatizo mengine ni mazingira magumu ya kufundisha na uhaba wa walimu. “Kinachotakiwa wajipange kufanyia kazi changamoto hizi zilizopo badala ya kuunda tume, wakati fedha nyingi tunasikia inapotea kwenye ubadhirifu,”alisema Profesa Mpangala.
Naye Profesa Maina alisema: “Hiyo tume ya kazi gani kwa sababu matatizo yanafahamika wazi, umewahi kusikia taifa gani ambalo halina mtalaa wa elimu. Hiyo ndiyo hali halisi kwa nchi yetu. ”
Kauli ya TAMONGSCO
Mwenyekiti wa TAMONGSCO, Mringo alisema: “Kwenye mitihani ya miaka ya nyuma, mtu alikuwa anaulizwa kwa mfano, taja sehemu tatu za mti. Akitaja mizizi, shina na matawi anakuwa amepata.”
Aliongeza: “Mwaka jana mtihani ulivyokuwa ni kwamba walikuwa wanatakiwa kutaja sehemu tatu za mti, halafu wanaambiwa waseme ni nini kinazunguka mti huo. Hapo ndiyo ilifanya mambo kuwa magumu.”
Mringo alisema mfumo huo umetokana na mtalaa mpya ambao unataka zaidi kuangalia uwezo tofauti na ule wa nyuma ambao uliwafanya wanafunzi wawe wanakariri zaidi, lakini akakosoa utaratibu wa kuanza kutumika kwake bila watahiniwa kufundishwa.
Kwa mujibu wa Mringo, ili watoto waweze kujibu aina hiyo ya maswali, inatakiwa waandaliwe kuanzia kwenye shule za msingi.
Alisema pia kuwa, mwaka huu alama za maendeleo ya mwanafunzi katika mitihani ya shule (continuous assessment) hazikutumika kama miaka mingine ambayo alama hizo zilikuwa zikichangia kwa asilimia 40 katika mtihani wa mwisho.
Mringo alizitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na wizi na udanganyifu wa mtihani ulidhibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Naye Mapunda alisema:“ Mtihani wa mwaka jana ulikuwa unapima zaidi uwezo wa watoto kuelewa siyo kukariri. Miaka ya nyuma watoto walikuwa wanaogopa zaidi mitihani ya ndani ya shule kuliko ile ya nje, ukiwaambia wasome kwa ajili ya mtihani wa taifa wanasema haina shida siyo migumu na kuwa ile ya ndani ndiyo ilikuwa migumu zaidi.”
Necta na Mulugo
Msemaji wa Necta, Nchimbi alisema mfumo wa mitihani ulibadilika 2008 baada ya mtalaa kubadilika kwa kuondoa baadhi ya mada za masomo na kuweka mpya.
“Tangu 2008, mitalaa ya fizikia na kemia tu ndiyo haikubadilika, yenyewe ilikuja kubadilika 2011 na katika kipindi chote mitihani imekuwa ikitungwa kwa mfumo huo huo na hakuna watu waliolalamika,” aliongeza Nchimbi.
Naye Mulugo alisema kwa sasa watu wanatoa sababu nyingi na kuhadharisha kuwa ni vizuri wakaiachia tume iliyoundwa na Waziri Mkuu ifanye kazi yake.
Source: Mwananchi
1 comment:
kd 10
yeezy boost
air jordan 1
supreme
jordans
air jordan
bape outlet
yeezy shoes
kevin durant shoes
supreme clothing
Post a Comment