Wafuasi wa CCM wakimtimua kwa mawe mfuasi wa CHADEMA wakati wa vurugu hizo |
Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho hayo.
Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.
“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha
bendera hiyo kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze
kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza
kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.
Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).
Baadhi ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe na kuwapiga wenzao wa Chadema na kusababisha tafrani kubwa katika eneo hilo la mkutano.
Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah Mambo alisema kuwa tukio hilo limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo la Mwanga Baa kulikofanyika sherehe za chama chao (CCM).
“Kwanza wamechukua bendera yetu. Halafu
tumeshangazwa na CCM kuruhusiwa kufanya maadhimisho yao wakati kuna
agizo la Mkuu wa Mkoa na polisi kukataza mikusanyiko ya kisiasa wakati
wa Bunge.
“Kwa nini sisi (Chadema) tuzuiwe mikutano yetu
wakati wenzetu wanafanya? Huku si kutenda haki....Tulikuwa na mikutano
ya kuimarisha chama katika kata kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili,
lakini tumezuiwa na tukaheshimu mamlaka,” alisema katibu huyo.
Pia tulikuwa tufanye mkutano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini tukazuiwa na tuliheshimu amri hiyo, alisema.
Mambo alisema katika vurugu hizo wafuasi wawili wa Chadema; Idd Kizota na Anord Swai waliumizwa na kushonwa nyuzi saba usoni.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya alisema hana taarifa za majeruhi hao.
“Ni vigumu kujua, unless (isipokuwa) wafike hospitalini
wakisindikizwa na kundi la wafuasi wenzao waliokuwa kwenye sare. Kama
walikuja kama wagonjwa wengine sio rahisi sana kwangu kujua,” alisema Dk
Mpuya.
Kumi mbaroni
Vurugu hizo zilizosababisha watu wawili kuumizwa
vibaya, zililazimisha Jeshi la Polisi kuwatia mbaroni watu kumi
wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alikiri kutokea vurugu hizo, lakini akasema bado anafanyia kazi suala hilo.
Kamanda Misime alikiri Serikali mkoani Dodoma kuzuia mikutano ya kisiasa wakati wa Bunge, lakini akasema kwa CCM ni tofauti kwa kuwa hizo ni sherehe zao za kuzaliwa kwa chama.
“Ninasoma hapa magazeti yenu, mmeandika wenyewe
maadhimisho ya miaka 36. Sasa hawa wanaadhimisha hiyo miaka 36 na siyo
mkutano wa kisiasa...Tulichokataza ni maandamano, misafara ya pikipiki
na kufanya mikutano ya siasa,” alisema Misime.
Akihutubia katika mkutano huo baada ya hali kutulia mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyangwine aliwakandia wapinzani na kusema kuwa wanachokifanya ni kuendeleza vurugu nchini na hawana sera ya maendeleo.
“Hivi jamani, hii leo hawa jamaa watasema nini?
Kama suala la barabara, leo hii unaweza kutoka Mtwara hadi Mwanza kwa
baiskeli, kama maji, michakato inafanyika, kama umeme ndiyo usiseme,
hivi wanataka nini?
“Hawa jamaa wamezoea kufanya vurugu...Si mmeona
wenyewe hapa, hawana lolote zaidi ya kufikiria vuru, wananchi msikubali
kuhadaiwa,”alisema.
JK akemea mifarakano
Akizungumza mkoani Kigoma kulikofanyika
maadhimisho hayo kitaifa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete,
alikemea siasa za makundi ndani ya chama, akisema tabia hiyo haijengi.
“Mifarakano ndani ya chama inayopaliliwa na viongozi ndani ya chama, inakibomoa chama na ndiyo maana tumepoteza majimbo matano katika uchaguzi uliopita,” alisema.
Source: Habari na Picha kwa hisani ya Mwananchi
No comments:
Post a Comment