Mchakato wa marekebisho ya kanuni za Bunge umeibua mjadala mkali baina ya wabunge, huku wengi wao wakieleza kuwa hatua hiyo ina lengo la kulifanya Bunge kukosa meno ya kuisimamia Serikali.
Miongoni mwa mambo yaliyozua mvutano katika kikao cha awali cha wabunge wote ni suala la muda wa wabunge kuchangia bungeni na jinsi wanavyotakiwa kupangwa kulingana na idadi yao kwa kila chama.
Bunge linakusudia kuwasilisha azimio la kutaka kubadili kanuni ambazo zilitarajiwa kuwasilishwa na Naibu Spika jana bungeni, lakini kutokana na baadhi ya mapendekezo kupingwa, hatua hiyo iliahirishwa hadi leo.
Mabadiliko hayo ni muhimu kabla ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuwasilishwa leo, kwani baadhi yake yanalenga kuwezesha mfumo mpya wa Bunge wa kuanza na Bajeti za wizara na baadaye kumalizia na Bajeti Kuu ya Serikali.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika juzi jioni na kuendelea jana, wabunge karibu wote walipinga pendekezo la kamati ya kanuni la kutaka kupunguza muda wa mbunge kuchangia mjadala kutoka dakika 15 zinazotajwa kwenye kanuni ya sasa Kifungu cha 62 (1) hadi dakika 10.
Suala jingine ambalo limeingizwa kwenye kanuni na ambalo limekuwa linapendekezwa na wabunge wa CCM la kutaka wabunge wapate nafasi za kuzungumza kulingana na idadi yao katika kila chama.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya kikao hicho kimesema endapo suala hilo litapitishwa, kulingana na mgawanyo wa wabunge kivyama, itabidi wazungumze wabunge wa CCM zaidi ya 10 ndipo apate nafasi mmoja kutoka kambi ya upinzani.
Pia wabunge katika kanuni mpya, wakati wa kujadili bajeti hawataruhusiwa kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa suala hilo ambalo lilizua mvutano kutokana na kuungwa mkono na wabunge wa CCM, huku likipingwa na wabunge wa upinzani, linaelekea kupitishwa kutokana na wingi wa wabunge wa chama tawala.
Kutokana na mjadala huo, ilibidi mambo mengine yarejeshwe kwenye kamati ya kanuni ili kufanyiwa marekebisho kutokana na ushauri wa wabunge.
Masuala mengine ni katika majukumu ya kamati za Bunge ambayo yakipitishwa kamati hizo hazitaweza kufuatilia sera ya ubinafsishaji wala kufanyia tathmini mashirika ya umma kwa kuwa vifungu vilivyokuwa vinaruhusu hali hiyo kwenye nyongeza ya nane, kifungu cha 13 havikuingizwa katika mapendekezo mapya.
“Kwa jumla kanuni hizi mpya zinapendekeza kamati za Bunge zisiwe zinatoa maagizo, bali zitoe ushauri na hii ni sawa na kuling’oa meno Bunge,” kilisema chanzo kingine.
Source:Mwananchi
No comments:
Post a Comment