Kushikiliwa kwa Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kumeendelea kuibua sokomoko baina ya polisi kwa upande mmoja na wafuasi wa Chadema na familia yake kwa upande mwingine.
Lema aliyekamatwa usiku wa manane kuamkia Ijumaa wiki hii, alihojiwa kwa saa tatu mfululizo katika Kituo Kikuu cha Polisi, Arusha lakini alinyimwa dhamana kwa maelezo kwamba kuachiwa kwake kungehatarisha amani.
Wakati hayo yakiendelea, askari katika kituo anakoshikiliwa Lema jana asubuhi walivutana vikali na ndugu wa mbunge huyo pamoja na uongozi wa Chadema Mkoa wa Arusha baada ya kumpa dakika moja kunywa chai aliyoletewa na kukataa asipewe dawa ya meno kutoka kwa mkewe, Neema.
Habari ambazo gazeti la Mwananchi lilizipata zinasema kutokana na hali hiyo, uongozi wa Chadema ulilazimika kumtuma wakili wa Lema, Method Kimomogoro kwenda Kituo cha Kati cha Polisi Arusha kujua sababu za polisi kufanya hivyo.
Mmoja wa ndugu wa Lema alisema polisi walimpa mbunge huyo dakika moja tu kunywa chai na kwamba muda huo ulipokwisha walimwongezea dakika nyingine tatu na kwamba zilipomalizika walimwamuru arejee mahabusu.
Wakati polisi wakifanya hivyo, tayari walikuwa wamekataa asipewe dawa ya meno aliyopelekewa na mkewe, Neema na kwamba matukio hayo yalizua mvutano mkali baina yake (Lema) na polisi waliokuwa kituoni hapo.
Wakili wa Lema, Humphrey Mtui alisema mahojiano ya mteja wake na polisi yalidumu kwa zaidi ya saa tatu kuanzia saa 7:50 mchana hadi saa 11:15 jioni, na kwamba walitaka ufafanuzi kwenye hoja tatu walizodai kwamba zilijengwa kwenye kauli alizotoa Lema wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA).
Maneno hayo yanayotafsiriwa na polisi kuwa ni uchochezi ni pamoja na “Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote duniani ni woga” na “Nimepata taarifa kuwa ndani ya dakika 15 Mkuu wa Mkoa atafika, asipofika ndani ya muda huo nitawaongoza kwenda kudai haki yenu ya msingi ya kupatiwa ulinzi.”
Kauli nyingine ni “Hawa ndio viongozi wetu (akimaanisha mkuu wa mkoa), tunaowategemea wanakuja kwenye matatizo wakijivuta utafikiri wanakwenda kwenye send-off.”
Lema anadaiwa kutamka maneno hayo baada ya Mulongo kugoma kuzungumza na wanafunzi kisha kurejea ndani ya gari akitaka viwepo vipaza sauti, kitendo kilichowafanya wanafunzi kuanza kumzomea kabla polisi kuanza kulipua mabomu ya machozi na kumwondoa eneo la tukio mkuu huyo wa mkoa.
Lema na Mulongo wote walikwenda IAA kutokana na tukio la kuuawa kwa kuchomwa kisu kwa aliyekuwa mwanafunzi wa taasisi hiyo, Henry Kago.
Baada ya vurugu hizo Mulungo alimtuhumu Lema kuandaa mazingira ya yeye kuzomewa .
Mdee, Nassari kukutana na Mulongo
Katika hatua nyingine, wabunge wawili wa Chadema, Halima Mdee (Kawe) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki) kesho wamepanga kwenda kuonana na Mulongo kuzungumza naye kuhusiana na kilichotokea IAA na kusababisha kukamatwa kwa Lema.
Nassari aliliambia gazeti hili jana kwamba wameamua kutoka Dodoma hadi Arusha kwa ajili ya “kushughulikia suala hilo.”
“Jumatatu tunatarajia kuonana na mkuu wa mkoa na tayari nimempa taarifa. Tunataka kuzungumza naye kilichotokea na hali ya kisiasa kwa sasa Arusha,”alisema Nassari.
Alisema wao kama wabunge, hawawezi kukaa kimya wakati kunaonekana kuna mgogoro baina ya mkuu huyo wa mkoa na mbunge mwenzao, Godbless Lema ambao unakiuka haki za kibinadamu.
“Tutazungumza naye na tutatoa ushauri wetu …na mimi kama mbunge wa Mkoa wa Arusha, nadhani nina nafasi ya kushauriana na mkuu wa mkoa kuhusiana na hali ya mambo ilivyo sasa Arusha,”alisema Nassari na kuongeza:
“Kabla ya kuonana na mkuu wa mkoa, tutajitahidi kuonana na polisi pia kuhusiana na kesi ya Lema na tunataka sisi kama wabunge tuwe sehemu ya wadhamini wa Lema.”
“Kabla ya kuonana na mkuu wa mkoa, tutajitahidi kuonana na polisi pia kuhusiana na kesi ya Lema na tunataka sisi kama wabunge tuwe sehemu ya wadhamini wa Lema.”
Hata hivyo, juhudi za kumpata jana mkuu wa Mkoa wa Arusha, kuelezea kama amepokea ujumbe kutoka kwa wabunge hao, zilishindikana kutokana na kuwa katika mapokezi ya marais watano wa nchi za Afrika ya Mashariki.
Chadema kumzomea RC
Katika hatua nyingine, Chadema mkoani Arusha kimeahidi kwamba kitaendeleza zomeazomea kwa mkuu wa mkoa huo, Mulongo kila watakapomwona kwenye matukio na shughuli zote za kijamii.
Katika hatua nyingine, Chadema mkoani Arusha kimeahidi kwamba kitaendeleza zomeazomea kwa mkuu wa mkoa huo, Mulongo kila watakapomwona kwenye matukio na shughuli zote za kijamii.
Katibu wa Chadema, Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema wafuasi wa chama hicho wataendelea kumzomea Mulongo kila watakapomwona hadi pale atakapobadilika kifikra, kimwenendo, maneno na vitendo kuhusiana na uhalali wa Chadema na viongozi wake katika uongozi wa umma waliokabidhiwa kisheria.
“Kama kupigiwa makofi na kushangiliwa anapofanya vyema kazi yake,
vivyohivyo mkuu wa mkoa ategemee kukumbana na zomeazomea kubwa kuliko aliyopata Uhasibu iwapo hatabadilika kiutendaji kwa kufanya kazi za kisiasa badala ya kuhudumia umma wote bila kujali tofauti za kiitikadi kisiasa,” alisema Golugwa.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment