Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na BungeWilliam Lukuvi |
KAULI YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU TAARIFA
YA AWALI YA TUME YA TAIFA YA KUCHUNGUZA MATOKEO
YA MTIHANI WA TAIFA WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa
Spika,
kwa mujibu wa Kanuni ya 49(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka
2007, naomba kuwasilisha Taarifa ya Awali ya Tume ya Taifa ya kuchunguza
matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012.
2.
Mheshimiwa
Spika,
Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne
mwaka 2012 yalionesha kuwa kiwango cha ufaulu kimeshuka kwa kiwango kikubwa
ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni. Matokeo yaliyotangazwa mwezi
Februari, 2012 yalionesha kwamba kati ya Wanafunzi 367,756 waliofanya mtihani huo, Watahiniwa 126,847 ndio waliofaulu. Katika idadi
hii, Wanafunzi waliofaulu katika Daraja la
Kwanza hadi la Tatu ni 23,520, sawa na Asilimia 6.4
na Daraja la Nne ni 103,327, sawa na Asilimia 28.1. Watahiniwa 240,909, sawa na Asilimia 65.5
ya Wanafunzi wote waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012 walipata
Daraja la Sifuri.
3.
Mheshimiwa Spika, kushuka kwa kiwango
cha ufaulu kulihusu shule za aina zote, yaani Sekondari za Serikali ikijumuisha
zilizojengwa kwa nguvu za Wananchi, Shule Binafsi na Seminari. Takwimu
zinaonyesha kwamba ukilinganisha matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2011 na mwaka
2012, Shule za Wananchi matokeo yao yameshuka kwa Asilimia 1.82; Shule za Umma za zamani (Kongwe) yameshukwa kwa Asilimia 6.43; Shule Binafsi yameshuka kwa
Asilimia 6.39; na kwa Shule za
Seminari yameshuka kwa Asilimia 7.29.
Hali hii inaonyesha kwamba, matokeo katika Shule
za Wananchi yameshuka kwa kiwango
kidogo ikilinganishwa na yale ya Shule
za Umma za zamani (Kongwe), Shule Binafsi na Shule za Seminari ambazo
zilitegemewa kufanya vizuri zaidi ya zile za Wananchi ambazo matokeo yao yameshuka zaidi kwa kati ya Asilimia 6.4 na 7.3.
4.
Mheshimiwa Spika, kutokana na matokeo
hayo yasiyoridhisha na ambayo yapo nje kabisa ya mwenendo wa ufaulu kwa miaka
ya karibuni, Serikali iliamua kuunda Tume ya Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha
Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka 2012 kwa madhumuni ya kupata
ufumbuzi wa kudumu.
HADIDU ZA REJEA
5.
Mheshimiwa
Spika, Tume
ya Uchunguzi ilipewa Hadidu za Rejea zikiwemo zifuatazo:
i.
Kubainisha sababu za matokeo mabaya ya
Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2012;
ii.
Kubaini sababu za kushuka kwa kiwango cha
ufaulu katika mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2011 hadi 2012;
iii.
Kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua
kukabiliana na tatizo la mwenendo wa kushuka kwa kiwango cha elimu mara moja,
kipindi cha muda mfupi, kati na kipindi cha muda mrefu;
iv.
Kutathmini nafasi ya
Halmashauri katika kusimamia Elimu ya Sekondari katika Halmashauri zake;
v.
Kuanisha sababu
nyingine zinazoweza kuwa zimechangia hali hii ya matokeo.
6.
Mheshimiwa Spika, katika kutafakari
Hadidu za Rejea hizo, Tume imejikita katika kujibu Maswali Makuu matatu.
i)
Kwa nini matokeo ya
Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008 yamekuwa na mserereko wa kushuka kuliko miaka
iliyotangulia?
ii)
Kwa nini Wanafunzi wa
Kidato cha Nne wa mwaka 2012 matokeo yao yalikuwa mabaya kuliko ya wenzao wa
mwaka 2011 pamoja na kwamba ufaulu ulishuka tangu mwaka 2008? na
iii)
Nini kifanyike.
WAJUMBE
WA TUME YA UCHUNGUZI
5.
Mheshimiwa
Spika, Tume
ya Uchunguzi iliongozwa na Prof. Sifuni Mchome kutoka Tume ya Vyuo Vikuu
Tanzania na ndiye alikuwa Mwenyekiti. Wajumbe wengine waliteuliwa kutoka Vyuo
vya Elimu ya Juu, Baraza la Wawakilishi, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Madhehebu ya Dini, Chama cha Walimu,
Muungano wa wenye Shule Binafsi na Muungano wa Walimu wa Sekondari. Orodha ya
Wajumbe wa Tume hiyo ni kama ifuatavyo:
NA.
|
JINA
|
TAASISI
ANAYOTOKA
|
NAFASI
|
1.
|
Prof.
Sifuni Ernest Mchome
|
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania
|
Mwenyekiti
wa Tume
|
2.
|
Mhe.
Bernadeta K. Mushashu (Mb.)
|
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
|
Makamu
Mwenyekiti
|
3.
|
Mhe.
Abdul J. Marombwa (Mb.)
|
Bunge
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
|
Mjumbe
|
4.
|
Mhe. Suleiman H. Hamisi (MBLW)
|
Baraza
la Wawakilishi Zanzibar
|
Mjumbe
|
5.
|
Mwalimu
Honoratha Chitanda
|
Chama
cha Walimu Tanzania (CWT)
|
Mjumbe
|
6.
|
Ndugu
Rakesh Rajani
|
TWAWEZA
|
Mjumbe
|
7.
|
Mwalimu
Daina W. Matemu
|
Umoja wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania
|
Mjumbe
|
8.
|
Mwalimu
Kizito Innocent Lawa
|
Taasisi
ya Elimu Tanzania
|
Mjumbe
|
9.
|
Mwalimu
Mabruki J. Makame
|
Baraza
la Elimu Zanzibar
|
Mjumbe
|
10.
|
Prof.
Mwajabu K. Possi
|
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
|
Mjumbe
|
11.
|
Mwalimu
Nurdin Mohamed
|
Chuo
cha Ualimu cha Al-Harmain
|
Mjumbe
|
12.
|
Ndugu
Peter Maduki
|
Baraza la Kikristo la Huduma za Jamii
|
Mjumbe
|
13.
|
Ndugu Mahmoud A. K. Mringo
|
Chama wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali
|
Mjumbe
|
14.
|
Ndugu
Abdallah H. Mohamed
|
Chuo
Kikuu cha Taifa Zanzibar
|
Mjumbe
|
TAARIFA
YA TUME YA UCHUNGUZI
6.
Mheshimiwa
Spika, tarehe
28 Aprili, 2013 Tume ya Uchunguzi wa Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012
ilikamilisha kazi yake katika Awamu ya Kwanza na kutoa Taarifa ya Awali.
Uchambuzi wa Taarifa hiyo ya awali unaonesha kuwa kutokana na Uchunguzi
uliofanyika, kwa muhtasari Tume imebaini mambo muhimu yafuatayo:
6.1
Matokeo ya Kidato cha Nne kuanzia mwaka 2008
yamekuwa na mserereko wa kushuka kuliko miaka iliyotangulia kwa sababu
mbalimbali ikiwemo changamoto zinazotokana na mafanikio yaliyopo sasa ya
kuongezeka sana kwa Idadi ya Shule za Msingi na za Sekondari, hususan kati
ya mwaka 2001 na sasa (2013); na hivyo
kuwa na idadi kubwa ya Wanafunzi waliopo Shuleni.
Kwa
mfano, katika kipindi cha mwaka 1961 hadi 2001 Idadi ya Wanafunzi wa Shule za
Msingi imeongezeka kutoka Wanafunzi 486,470
(1961) hadi 4,875,764 mwaka 2001,
sawa na ongezeko la Wanafunzi 4,389,294
katika kipindi hicho cha takriban miaka 40.
Hata hivyo, kati ya mwaka 2001 hadi 2012 Wanafunzi wameongezeka kutoka 4,875,764 mwaka 2001 hadi 8,247,472 mwaka 2012, sawa na ongezeko
la Wanafunzi 3,371,708 katika
kipindi cha takriban miaka 11 na
hivyo kufanya jumla ya Wanafunzi wote wa Shule za Msingi kuwa 8,247,472 mwaka 2012.
Kuhusu
Shule za Sekondari Idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka 11,832 mwaka 1961 hadi 289,699
mwaka 2001 ambayo ni sawa na ongezeko la Wanafunzi 274,867 katika kipindi hicho cha miaka 40. Lakini kati ya mwaka 2001 hadi 2012 Idadi ya Wanafunzi
imeongezeka kutoka 289,699 (mwaka
2001) hadi 1,884,270 mwaka 2012,
sawa na ongezeko la Wanafunzi 1,594,571
katika kipindi cha miaka 11 tu.
Juhudi hizi
zimetokana na Mipango mbalimbali iliyoandaliwa chini ya Mpango wa Maendeleo ya
Sekta ya Elimu wa mwaka 1999. Mipango hii ni pamoja na:
1.
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi
(MMEM) wa mwaka 2002 ambapo:
a)
MMEM I ambayo
ililenga katika kufungua Shule zaidi ili Wanafunzi wengi wa rika lengwa waweze
kujiunga na Elimu ya Msingi;
b)
MMEM II ambayo
ililenga katika kuboresha ubora wa elimu itolewayo katika Shule za Elimu ya
Msingi; na
c)
MMEM III ambayo
ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa Elimu ya Msingi baada ya
mafanikio ya MMEM I na MMEM II.
2.
Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari
(MMES) wa mwaka 2004 ambapo:
a)
MMES I ambayo
ililenga katika kufungua Shule zaidi za Sekondari katika ngazi ya Kata ili
Wanafunzi wengi zaidi wanaomaliza Elimu ya Msingi waweze kujiunga na Elimu ya
Sekondari Kidato cha Kwanza; na
b)
MMES II ambayo
ililenga katika kuendelea kuimarisha ubora wa Elimu ya Sekondari kadri Idadi ya
Wanafunzi wa Elimu ya Sekondari wanavyoendelea kuongezeka.
Changamoto
zinazoambatana na mafanikio haya ni pamoja na mazingira yasiyoridhisha ya
kufundishia na kujifunzia, ikiwemo upungufu wa miundombinu muhimu ya shule kama
vile Madarasa, Maabara, Madawati, Maktaba, Nyumba za Walimu, Hosteli na majengo
mengine muhimu ya Shule. Vilevile, kuna tatizo la uhaba wa Walimu, Vitabu, zana
za kufundishia na matatizo ya Ukaguzi wa Shule. Vilevile, Tume imebaini kuwa
Mfumo wa Elimu ya Msingi na Sekondari unakabiliwa na changamoto nyingine
mbalimbali ambazo Taifa inapitia kwa sasa ikiwemo masuala ya Kisera, Kisheria,
Kimfumo, Kimuundo pamoja na changamoto za uhaba wa Rasilimali Fedha na Rasilimali
Watu. Tume inaendelea kufanyia kazi maeneo haya kwa kushirikiana na Wataalamu
na Wadau wengine;
6.2
Kuhusu matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2012,
Tume imebaini kwamba, pamoja na Wanafunzi hawa kuwa katika
mazingira yanayofanana na ya wenzao
wa miaka
iliyopita na kwamba ufanisi katika shule kwa ujumla
umekuwa unashuka kwa sababu mbalimbali,
ufaulu wao umeshuka zaidi kwa sababu ya mabadiliko ya
mchakato wa kuandaa na kutoa matokeo ya mtihani kwa mwaka 2012. Mfumo uliotumika mwaka 2012 katika kupanga matokeo na madaraja ni tofauti
na ule uliotumika mwaka 2011 na miaka iliyotangulia. Uchunguzi unaonesha kuwa
mwaka 2011, Baraza la Taifa la Mitihani lilikuwa linachakata Alama za mwisho kwa kutumia mfumo ambao ulikuwa unabadilika
kutegemea hali ya ufaulu wa Mwanafunzi
ambao ni “National Mean Difference” (NMD). Utaratibu huu ulitokana na tofauti
ya Wastani wa Kitaifa wa Alama za Maendeleo kutoka Alama za Maendeleo Endelevu
(Continued Assessment – CA) za
Watahiniwa wote na Wastani wa Kitaifa wa ufaulu wa Mitihani ya mwisho kwa somo
husika. Kila Mtahiniwa aliongezewa “National
Mean Difference” iliyokokotolewa katika Alama za Mtihani wa mwisho ili
kupata Alama itakayotumika kupata Daraja la ufaulu. Kimsingi, kila somo
lilikuwa na NMD yake kulingana na Continued
Assessment (CA) zilivyo kwa mwaka husika.
Lakini mwaka 2012 Baraza lilitumia Mfumo Mpya ambao ulikuwa haubadiliki
kutegemea hali ya ufaulu wa Mwanafunzi, yaani kuwa na Viwango Maalum vya
Kutunuku (Fixed Grade Ranges). Tume
imebaini kwamba, pamoja na kwamba Mfumo huo uliandaliwa kwa nia nzuri,
Utaratibu huo mpya haukufanyiwa utafiti na maandalizi ya kutosha kabla ya
kutumika.
MAPENDEKEZO YA AWALI YA TUME
7.
Mheshimiwa
Spika,
kwa kuzingatia masuala mbalimbali yaliyojitokeza wakati wa uchunguzi, Tume
katika Taarifa yake ya awali imetoa mapendekezo mbalimbali yakiwemo yale
yanayohitaji kutekelezwa kwa haraka. Kutokana na kuwepo kwa mapendekezo hayo
ambayo inabidi yafanyike kwa haraka, tarehe 29 Aprili, 2013 Baraza la Mawaziri
lilipokea Taarifa ya Awali ya Tume na kuijadili ambapo liliridhia mapendekezo
hayo yaanze kutekelezwa mara moja. Maamuzi hayo ya Baraza la Mawaziri yanalenga
kutenda haki kwa Walimu na Wanafunzi ambao juhudi zao za kufundisha na
kujifunza zimepimwa kwa kutumia Mfumo mpya ambao hawakupata fursa ya
kushirikishwa na kuandaliwa. Mapendekezo hayo ni yafuatayo:
i.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka
2012 yafutwe na yaandaliwe upya kwa
kutumia utaratibu uliotumika mwaka 2011;
ii.
Standardisation ifanyike
ili matokeo ya Wanafunzi yalingane na juhudi walizoziweka katika kusoma kwa
mazingira na hali halisi ya Tanzania na uamuzi wa Taifa kuongeza idadi ya Shule
na Wanafunzi wakati uwekezaji katika ubora unaendelea;
iii.
Baraza la Taifa la Mitihani limeelekezwa
kuzingatia kuwa pamoja na kwamba Sheria ya kuanzishwa kwake inawaruhusu kufanya
marekebisho ya mchakato wa mitihani, lakini marekebisho yoyote ya kubadilisha
Utaratibu wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya Mitihani, lazima yahusishe Wadau wote wanaohusika na
Mitaala, Ufundishaji na Mitihani.
Wakati
Tume inaendelea kukamilisha kazi yake, uamuzi wa Baraza la Taifa la Mitihani wa
kutumia utaratibu mpya wa kupanga viwango vya ufaulu na madaraja ya matokeo ya
Mitihani uliotumika mwaka 2012 usitishwe
na badala yake Baraza la Mitihani litumie Utaratibu wa mwaka 2011 kwa Kidato cha Nne na cha Sita kwa
Mitihani yote ukiwemo utaratibu wa Standardization
na kutoa Matokeo mapya kwa kuzingatia maelekezo haya.
Aidha,
mchakato wa Mfumo wa Tuzo wa Taifa (National
Qualifications Framework) na Mfumo wa kutahiniwa/kutathmini maendeleo ya
Mwanafunzi katika masomo yake (National
Assessment Framework) ukamilishwe haraka iwezekanavyo.
UTEKELEZAJI
WA MAPENDEKEZO YA TUME
8.
Mheshimiwa
Spika, kutokana
na umuhimu wa mapendekezo hayo, Baraza la Mawaziri limeamua kwamba utekelezaji
wa mapendekezo hayo uanze mara moja.
9.
Mheshimiwa
Spika,
Tume ya Uchunguzi itaendelea kukamilisha Taarifa yake vizuri kwa kuhusisha
Wadau mbalimbali ili kupata maoni zaidi na ushauri wao juu ya mambo mbalimbali
yaliyobainika wakati wa uchunguzi kabla ya kuikamilisha na kuitoa kwa matumizi
ya Umma na Vyombo mbalimbali.
HITIMISHO
10.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inaipongeza sana Tume kwa kutoa mapendekezo ya awali ambayo Serikali
imeyaridhia. Aidha, Serikali inawashukuru Wananchi wote na Wadau mbalimbali wa
Sekta ya Elimu wanaoendelea kutoa maoni na ushauri wao kwa Tume.
11.
Mheshimiwa
Spika,
Serikali inawahakikishia Wananchi kuwa itaendelea kuboresha Elimu Nchini ili
kuwezesha Watoto wetu wapate mafanikio katika maisha na maendeleo yao, kwani
Wahenga wanasema “Elimu ni Ufunguo wa
Maisha”.
12.
Mheshimiwa
Spika,
naomba kuwasilisha.
No comments:
Post a Comment