CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeazimia kufanya maandamano ya amani Juni 29, mwaka huu, kwenda Ikulu kuonana na Rais Jakaya Kikwete, hata kama watazuiwa na Polisi. Lengo la maandamano hayo, kwa mujibu wa chama hicho, ni kumfikishia malalamiko yanayohitaji hatua za haraka, ili nchi iweze kuendelea kuwa na amani, utulivu, mshikamano na upendo.
Kutokana na hilo, kimesisitiza kuandamana, hata kama Jeshi la Polisi litayazuia kwa sababu zozote zile, zikiwamo za ujio wa Rais wa Marekani, Barrack Obama au kisingizio chochote.
Pamoja na hilo, kimesema kuwa kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyoitoa hivi karibuni bungeni ya kwamba wananchi wanaokiuka sheria wapigwe tu, itadhihirika siku hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Siasa wa chama hicho, Shaweji Mketo, alisema maandamano hayo yana lengo la kumfikishia Rais Kikwete ujumbe juu ya vitendo vya ukatili, wizi, ubakaji vinavyofanywa na polisi.
Alieleza kuwa watamfikishia Rais Kikwete, ujumbe wa kukataa kuundwa kwa tume mbalimbali za kuchunguza matukio yaliyotokea Mtwara na Arusha.
Kwa mujibu wa Mketo, malalamiko hayo yanayopelekwa kwa Rais Kikwete ni ya msingi kwa taifa na yasipotatuliwa mapema, yanaweza kuifikisha nchi pabaya.
“Itakumbukwa wakati Chadema kinahitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kule Arusha, kulitokea mlipuko wa bomu na kusababisha vifo na majeruhi, sasa cha ajabu tume zimeundwa kuchunguza, tunasema si mara ya kwanza kwa tume kuundwa, lakini hakuna majibu.
“Tumeona njia nzuri ya kufikisha ujumbe ni kwenda kwa Rais Kikwete kumfikishia ujumbe huu na tayari tumemwandikia barua pamoja na Jeshi la Polisi, sasa kumekuwapo na vizuizi kadhaa tunapoandaa maandamano, tunasema hatutarudi nyuma kwa hilo.
“Na leo (jana) baadhi ya viongozi wa CUF wameitwa Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa Kova ili kuzungumza suala hilo, tunasema msimamo wetu ni huo na tunataka kauli ya Pinda ya kutoa kibali kwa polisi kupiga, itadhihirika siku hiyo na ujio wa Obama hauwezi kutuzuia kufanya shughuli zetu,” alisema.
Akizungumzia sakata la gesi ya Mtwara, alisema wameshangazwa na baadhi ya viongozi serikalini kudiriki kupotosha umma, kwamba wananchi wa mikoa hiyo hawataki nishati hiyo iondoke mkoani humo, jambo ambalo si kweli.
Alisema wananchi wa Mtwara wanataka kujua namna watakavyonufaika kwanza na nishati hiyo, kutokana na ushahidi uliopo katika migodi mingine, ikiwamo ya Geita.
“Pamoja na upotoshwaji huo wa gesi ya Mtwara, CUF inashangazwa na kitendo cha JWTZ, ambalo limeonekana awali kutenda haki kwa wananchi baada ya wananchi kukosa imani na polisi kutokana na wizi, uchomaji wa nyumba, maduka na masoko, lakini jeshi hilo limeingia katika mkumbo wa kuwatesa raia bila makosa.
“JWTZ, wiki hii limemteka Mkurugenzi wa Siasa wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Saibogi na kumpeleka katika kambi ya Nanyamba na kumvua nguo na kumpiga mijeledi usiku kucha bila hatia, ambapo asubuhi lilimuachia na kuwakamata viongozi wengine 39 wa chama hicho na kuwafanyia vitendo hivyo bila kuwafungulia mashitaka.
“Tulikianzisha CUF kwa madhumuni ya kuwaunganisha Watanzania wote popote walipo bila kujali itikadi zao na waweze kukataa aina yoyote ya uonevu, ukandamizaji, unyanyasaji na ubaguzi na ndio lengo la kukataa haya yanayotokea sasa,” alisema Mketo.
Alisema kuwa uvumilivu wa wananchi wanyonge unakaribia kwisha na sasa wanahitaji kukombolewa na si kukandamizwa, huku akisisitiza kuwa CUF kipo tayari kuendeleza mapambano ya kudai haki sawa kwa Watanzania wote.
Mketo alisema maandamano hayo yana lengo la kuilazimisha Serikali kukaa pamoja na kuwasikiliza wananchi wa Mtwara, ili kujua hoja zao na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusiana na gesi.
Alisema maandamano hayo yataanzia Kituo cha Buruguruni Sheli, saa nne asubuhi na kupita Barabara ya Uhuru, Mnazi Mmoja, Bibi Titi, Posta Mpya, Ardhi hadi Ikulu na yataongozwa na Mweyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba na viongozi wengine wa ngazi za juu, wakiwamo wabunge.
Alieleza kuwa kuanzia leo, wanaanza mikutano ya hadhara ya kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye maandamano hayo.
No comments:
Post a Comment