Sunday, June 23, 2013

Mbunge wa CCM na CHADEMA kidogo wazichape kavu kavu


Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba jana nusura wachapane makonde baada ya kutupiana maneno ya kashfa, wakituhumiana kuhusika na mlipuko wa bomu uliotokea Jumamosi iliyopita mkoani Arusha.
Tukio hilo lilitokea katika viwanja vya Hoteli ya St Gasper nje kidogo ya mji wa Dodoma, walipokwenda kwa ajili ya kuhudhuria semina ya wabunge wapambanaji na Ukimwi, ambapo baadhi ya wabunge wa Chadema walihudhuria, baada ya kutoonekana mjini humo tangu Juni 17 mwaka huu.
Wabunge hao wa Chadema hawakuhudhuria kikao chochote cha Bunge kutokana na kwenda mkoani Arusha kwa shughuli mbalimbali, kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wao wa kuhitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika viwanja vya Soweto, Juni 16 jijini humo.
Malumbano hayo yanatokana na Nchemba kuituhumu Chadema kuhusika na mlipuko huo, Juni 20 mwaka huu wakati akichangia hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2013/2014, akisema chama hicho kilipanga kulipua bomu hilo ili kuwafanya Watanzania waamini kuwa Serikali ya CCM ndiyo inayohusika na tukio hilo.
Ilivyotokea
Wakati Msigwa akiingia katika ukumbi huo akiwa ameongozana na Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje, walikutana uso kwa uso na Nchemba ambaye alikuwa akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Said Amour Arfi.
Baada ya Nchemba kumwona Msigwa alimkaribisha mchungaji huyo akisema; “Karibu sana bwana, salama lakini?”
Hata hivyo, badala ya kujibu salamu hiyo ya Nchemba, Msigwa alikuja juu na kumtuhumu Nchemba kwamba anatoa kauli zinazoweza kuvuruga amani ya nchi.
“Wewe ni mtu hatari sana, haya yote yanasababishwa na wewe, mnatumia damu za watu kutafuta madaraka,” alisema Msigwa akimtupia maneno Mwigulu.
Baada ya kauli hiyo Nchemba alihoji akisema: “Ki-vipi? Hayo mambo tuyaache, Msigwa achana na haya mambo!”
Baada ya Nchemba ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM kujibu, Msigwa alimsogelea karibu na kumnyooshea kidole, huku akiendelea kumtuhumu kuwa ana siasa chafu zinazopandikiza chuki kwa jamii.
Malumbano hayo pia yaliingiliwa na Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere ambaye alimuunga mkono Msigwa, huku akimtuhumu Nchemba kuwa ni mtu mbaya katika siasa za Tanzania. Katika kile kilichoonekana kutaka kuweka mambo sawa, Wenje alimvuta Msigwa na kumpeleka ukumbini ili kuepusha shari baada ya wabunge hao kuzidi kurushiana maneno.
Hata walipoingia ndani ya ukumbi huo wabunge hao waliendelea kulumbana, lakini wakatulizwa na baadhi ya wabunge waliokuwa karibu yao.
Alipotakiwa kueleza sababu za mzozo huo na Nchemba, Mchungaji Msigwa alisema, “Achana na yule mpuuzi, mimi siwezi kuzungumza na mtu mnafiki, mkatili na yeye ndiye alihusika na mipango mibaya dhidi ya Chadema hata mlipuko wa Arusha hivyo kutesa watu wa Chadema.”
Alisema kuwa yeye haoni sababu ya mtu mwenye mipango mibaya na wananchi wa Tanzania pamoja na chama chake (Chadema), kuwafuata na kujikomba.
Kwa upande wake Nchemba alipoulizwa alisema kuwa alichokizungumza ni mtazamo wake na kwamba ikiwa kuna mtu anayeona kuwa alizungumza uzushi, ajitokeze na kupinga. “Nilichokizungumza ndicho kilichofanyika kwa matukio yote niliyoeleza bungeni,”alisisitiza Nchemba.
Alichokisema bungeni
Wakati akichangia mjadala wa Bajeti, Nchemba alisema hata ripoti iliyotolewa na Jukwaa la Wahariri baada ya kutekwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Absalom Kibanda, ilieleza kuwa watu waliohojiwa walidai kuwa Chadema kimepewa mafunzo kutoka nje ya nchi, kwamba kikitumia baadhi ya viongozi wa dola wasiokuwa waaminifu kuteka watu na hata kuua watu maarufu, watu wataamini CCM imeshindwa kuongoza nchi na sasa imeanza kuua watu.
“Hii ni taarifa ya Jukwaa la Wahariri na sehemu ambayo kuna maneno hayo ipo katika ukurasa wa nane wa ripoti hiyo” alisema.
Alisema Chadema kimewahi kumvalisha raia nguo za polisi ili aonekane ni askari wa jeshi hilo na kwamba hata mlipuko wa Juni 16, pia inawezekana chama hicho kilimvalisha mtu nguo za polisi ili ionekane kuwa polisi ndiyo alihusika na ulipuaji wa bomu.
“Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa kijana anayedaiwa kuuawa na polisi mkoani Morogoro, aliuawa baada ya kupigwa risasi na Chadema ili kuonyesha kuwa serikali ya CCM inakandamiza upinzani,” alisema.
Akizungumzia mkanda wa video unaoonyesha tukio la mlipuko wa bomu la Arusha, Nchemba alisema kuwa tukio hilo lilipangwa na ndiyo maana Chadema walipanga hadi wakarekodi tukio hilo.
“Lile tukio limepangwa na ndiyo maana hata aliyechukua ile video hakustushwa kabisa na mlipuko wa bomu, jambo hilo haliwezekani kabisa, tukio lile limepangwa kwa kiwango cha chini kabisa,” alisema na kuongeza; “Mtu yule alikuwa akichukua video utadhani yuko katika harusi,
CCM haijashiriki katika tukio la Arusha, ila kutokana na nguvu ya chama hiki ni lazima kitahusishwa na tukio hilo.”
Source: Mwananchi

No comments: