Freeman Mbowe |
Mbowe alifika Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam kuitikia wito wa jeshi hilo kumtaka awasilishe ushahidi wake aliosema kuwa anao, lakini aligoma akisema atautoa pale tume ya kijaji itakapoundwa na Rais Jakaya Kikwete kama alivyoomba.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika alisema jana kuwa Mbowe alikwenda polisi baada ya kuandikiwa barua ya kumtaka afike kuwasilisha ushahidi. Alifika lakini aligoma kutoa ushahidi huo.
“Alikwenda tu kuitikia wito wa polisi uliomtaka awasilishe ushahidi, lakini amegoma kufanya hivyo na amewaeleza polisi kuwa hatafanya hivyo hadi Rais atakapounda tume ya kijaji kama alivyomwandikia barua,” alisema na kuongeza: “Anachosubiri sasa ni majibu ya Rais kuhusu barua yake.”
Mnyika alisema baada ya maelezo hayo, Mbowe alitakiwa kuyaweka kimaandishi kupitia kwa wakili wake Peter Kibatala na kuyawasilisha polisi ifikapo kesho.
Akizungumzia suala hilo, Wakili Kibatala alisema: “Mbowe ameachiwa baada ya majadiliano ya kisheria kati yangu na Kamanda Advocate Nyombi. Tumekubaliana kujibu kwa maandishi wito wa polisi walioutoa kwake wakimtaka awasilishe ushahidi wa kuhusika kwa polisi katika mlipuko wa bomu Arusha na kisha kuyafanyia kazi hayo kisha kutuarifu.”
Msemaji wa Polisi SSP, Advera Senso alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema anafuatilia kujua kama kweli Mbowe alihojiwa na kama kutakuwa na habari ya kuwajulisha wananchi ataitoa baadaye.
Wiki iliyopita jeshi hilo lilimhoji Mbowe kwa madai kuwa kauli zake alizozitoa baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho ni za uchochezi.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alihojiwa kutokana na madai aliyosema kwamba polisi ndiyo waliohusika na ulipuaji wa bomu Arusha, pia polisi kusaidia CCM kwenye uchaguzi na kumtuhumu Rais Jakaya Kikwete kuhusika na mauaji ya Arusha kutokana na kukaa kwake kimya.
No comments:
Post a Comment