Sunday, November 14, 2010

Waingereza waliotekwa Somalia waachiwa huru


Raia wawili wa Uingereza waliotekwa nyara na maharamia wa Kisomali wameachiliwa huru.
Paul na Rachel Chandler wameachiwa baada ya kukaa mateka kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kikombozi kutolewa.

Paul na Rachel ambao walionekana wadhaifu na wachovu, walisafirishwa kwa ndege kutoka Somalia kwenda Nairobi, Kenya, huku wakiwa hawajaumizwa na katika afya njema, kwa mujibu wa daktari aliyekuwa akiwatazama mara kwa mara nchini Somalia.

"Mbali na mateso ya kisaikolojia waliyopata kwa miezi 13 iliyopita, hali yao si mbaya sana," amesema Dk Mohamed Elmi Hangul.

Mkasa wa raia hao wa Uingereza ulianza Oktoba 23 mwaka jana, wakati chombo chao cha kifahari kikisafiri baharini kutoka Ushelisheli kwenda Tanzania. Ili kuepuka kutekwa nyara katika mwambao wa Somalia wawili hao walisafiri mamia ya maili upande wa kusini.

Hata hivyo hawakuweza kukwepa hilo. Watu wenye silaha waliingia ndani ya chombo chao cha baharini na kukiteka kwa nguvu.

Siku chache baadaye walipelekwa kwenye meli kubwa karibu na pwani ya Haradheere, huku meli ya Kivita ya Uingereza ikiwa karibu lakini ikishindwa kufanya lolote.

No comments: