Monday, December 20, 2010

Mashabiki TP Mazembe wafanya vurugu wapiga wachina




Ghasia zimezuka hapo jana katika mji wa Lubumbashi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya klabu ya mchezo wa soka ya TP Mazembe kushindwa katika fainali ya kuania kombe la dunia kwa klabu mjini, Abu Dhabi, usiku wa kuamkia Jumapili.

TP mazembe ambayo ilikuwa klabu ya kwanza kutoka barani Afrika kuwahi kufuzu kushiriki katika fainali ya mashindano hayo ilishindwa mabao 3-0 na klabu ya Inter Milan ya Italia.

Habari zinasema kuwa mashabiki ambao walikuwa na matumaini makubwa kwamba TP Mazembe ingeshinda mchuano huo waliingia katika barabara za mji wa Lubumbash na kuvamia biashara zinazomilikiwa na makampuni ya uchina.

Inaaminika kuwa mashabiki hao walidhani kuwa refa aliyesimamia mchuano huo raia wa Japan alikuwa mchina, na walikuwa wamekasirishwa na hatua alizochukuwa refa huyo dhidi ya TP Mazembe wakati wa mchuano huo.

Wakati wa ghasia hizo mali ziliporwa lakini polisi waliweza kuwatawanya mashabiki hao kwa kufyatua risasi hewani.

Makampuni mengi ya Uchina yanaendesha biashara katika mji wa Lubumbashi ambao ni kitovu cha uchimbaji wa madini ya shaba nyekundu.(BBC Swahili)

No comments: