Friday, April 22, 2011

Marekani kumtwanga Gaddafi Libya


Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Robert Gates amesema ndege za kivita zisizokuwa na rubani zinatekeleza mashambulizi ya anga nchini Libya.

Gates amesema utumizi wa ndege hizo uliidhinishwa na rais Obama na kwamba zitaongeza uwezo wa wanajeshi wa muungano wa NATO katika harakati zao za kijeshi nchini humo.

Waasi nchini Libya, wamekuwa wakipambana na wanajeshi wa Kanali Gadaffi tangu mwezi Februri mwaka huu, lakini wameanza kupiga hatua ndogo.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Washington, Gates amesema kwamba rais Obama aliidhinisha utumizi wa ndege hizo maalum zisizo na rubani kama mchango wao na pia kudhihirisha uwezo wao wa kijeshi.
Ndege za kivita za Marekani

Ndege za kivita za Marekani

Amesema ndege mbili zitakua chini ya usimamizi wa NATO kwa saa 24 kila siku.

Bwana Gates, amekanusha madai kuwa kutumwa kwa ndege hizo ni ishara ya Marekani ya kujiunga na Muungano wa NATO katika harakati zake za kijeshi nchini Libya, kwa njia ya siri.

Ndege hizo maalum za kurusha makombora zinatumika kuwalenga wapiganaji wa waasi katika mipaka ya Pakistan na Afghanistan.

Idara ya ulinzi ya Marekani imesema ndege hizo zitakuwa na uwezo wa kuwatambua wanajeshi wa Gadaffi ikiwa watajificha ndani ya magari ya kibinafsi au wakiingia kwenye maeneo ya makaazi ya watu.

Ndege hizo zina uwezo wa kupaa muinuko wa chini kuliko ndege zingine za kivita na hivyo kuifanya bora katika juhudi za kijasusi na kufanya mashambulio, kwa kuwa ni vigumu kwa ndege hizo kuonekana kwenye mtambo wa rada.

Wataalamu wanasema hii ni ishara tosha kuwa Marekani inajihusisha zaidi katika mzozo huo nchini Libya.

No comments: