photo
Waziri Mkuu Mstaafu Fededrick Sumaye
Kuna taarifa ambazo bado hazijathibitiswa kutoka Tanzania kuwa Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye leo anaongea na waandishi wa habari na kueleza kile kilicho moyoni mwake na huenda uamuzi kwamba atakihama Chama Cha Mapinduzi au la huenda akautoa.

Hata hivyo mkutano huo na waandishi wa habari bado ni kitendawili kwani hakuna vyanzo vya uhakika vilivyothibitisha mkutano huo lakini kuna taarifa za siri kuwa atafanya mkutano huo leo mjini Dar es Salaam katika hotel moja ambayo nayo jina lake halijawekwa wazi.

Lakini habari ambazo zimetufikia zinasema alitarajiwa kufanya mkutano huo katika hotel ya Courtyard ilipo mjini Dar es Salaam kuanzia saa 6 za mchana.

Baada ya kushindwa kinyang'anyiro cha Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM NEC kumekuwa minong'ono na taarifa ambazo zimenukuliwa na vyombo vya habari vya Tanzania  kuwa mwanasiasa huyo mkongwe ambaye ana mpango wa kugombea urais mwaka 2015, huenda akahamia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.

Wiki iliyopita kulikuwa na taarifa kuwa Sumaye alifanya mazungumzo na viongozi wa CHADEMA habari ambazo pia zilithibitishwa na kiongozi mmoja wa chama hicho ambaye hakupenda kutajwa jina lake.

Kama Sumaye leo atatangaza kukihama Chama Chama Mapinduzi atakuwa ni kiongozi wa kwanza ambaye amewahi kushika wadhifa wa juu wa Uaziri Mkuu kuhama chama Tawala na kwenda upinzani.

Wengine ambao waliwahi kushika nyazifa za juu na kukihama chama tawala cha CCM ni Maalim Seif Sharif Hamad ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa  Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kujiunga na Chama cha Wananchi CUF.

Mwingine ni Agustino Mrema ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu na kwa sasa ni Mwenyekiti wa chama TLP.

Tunaendelea kufuatilia taarifa hizi kwa karibu na tutakupasha zaidi kile kitakachoendelea na kama kweli kafanya mkutano huo au la.