Saturday, October 6, 2012

Kimbunga CCM baada ya Sumaye sasa Chikawe

Waziri wa Katiba na Sheria Mathias Chakawe
WIMBI la mawaziri na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kushindwa katika chaguzi ndani ya chama hicho, limeendelea kushika kasi, baada ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, kupigwa chini na kijana mdogo mwenye umri wa miaka 23, kwenye nafasi ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Waziri Chikawe ambaye pia ni Mbunge wa Nachingwea, aliingia katika uchaguzi kwa kujiamini, lakini alijikuta akiambulia kura 520 dhidi ya 780 za Fadhili Liwake.

Akitangaza matokeo hayo, msimamizi wa uchaguzi huo, Zakinai Msongo alisema, matokeo hayo ni halali kutokana na wajumbe kutumia haki yao ya msingi.

“Ndugu wajumbe napenda kuwatangazia matokeo haya, baada ya kazi kubwa mliyoifanya tangu asubuhi, mshindi wetu ni Fadhili Liwake, ambaye amefuatiwa na Mathias Chikawe na Fadhili Mkuchi, ameshika nafasi ya tatu,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, ukumbi mzima uliibuka kwa shangwe na kuacha Waziri Chikawe na wapambe wake wakiwa hawaamini kilichotokea.Lakini katika hali ya kushangaza, baada ya msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo hayo, Liwake alianguka chini na kupoteza fahamu ghafla.

“Huwezi amini ndugu yangu, baada ya kutangazwa mshindi, Liwake alianguka ghafla na kupoteza fahamu, jambo hili limeshangaza wajumbe waliokuwa ukumbini,” alisema mmoja wa wajumbe wa mkutano huo.Baada ya kuanguka, alikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea kwa ajili ya matibabu.

“Tumemkimbiza mshindi wetu hospitali kupata matibabu, watu hawaamini kilichomtokea, lakini tunamuomba Mungu amsaidie apone haraka, ili aanze majukumu yake mapya,” alisema mjumbe huyo.

No comments: