Wednesday, November 14, 2012

Mabadiliko Mengine CCM: Kinana Katibu Mkuu mpya

Katibu Mkuu mpya wa CCM Abrahaman Kinana

 Mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete amemteua Abrahaman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho kuchukua nafasi ya Katibu aliyemaliza muda wake Wilson Mukama.

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) kimekutana katika Ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya chama, maarufu kama Whitehouse mjini Dodoma,ambacho kimepitisha uteuzi wa Katibu Mkuu mpya pamoja na timu nzima ya Sekretarieti ya chama hicho.

 Kikao hicho kilijadili juu ya kuunda na kupitisha majina yaliyopendekezwa  na Mwenyekiti wa Chama  Jakaya Mrisho Kikwete, ya wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama ya Taifa (CC) pamoja na uundaji wa sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.



 Mwenyekiti wa Chama kwa mujibu wa Kanuni na Katiba ya Chama Cha Mapinduzi, anayo fursa ya kuteua wajumbe kumi(10) wa Halmashauri kuu ya Taifa, ambapo  Mwenyekiti aliwateua wajumbe wanne(4) na akabakiza nafasi nyingine sita (6) miongoni mwa wajumbe hao ni Mhe. Asha-rose Migiro, Mhe. Zakhia Meghji, Mhe. Nape nnauye na  Mhe. Abdulrahaman Kinana .

Baada ya uteuzi huo Mwenyekiti pia alipendekeza majina ya Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, ambapo alipendekeza majina yafuatayo;

  1. Nafasi ya Katibu Mkuu, alimpendekeza Mhe. Abdulrahaman kinana.
  2. Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar,  Mhe. Vuai Ali Vuai.
  3. Nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Bara, Mhe. Lameck Mwigulu Nchemba.
  4. Katibu wa Oganaizesheni ni Ndugu Mohamed Seif Khatibu.
  5. Katibu wa Siasa na Mahusiano ya Kimataifa, Asha-rose Migiro.
  6. Katibu wa Uchumi na Fedha, Zakhia A. Meghji. 
  7. Katibu wa Itikadi na Uenezi- Nape Nnauye
 Baada ya mapendekezo hayo, Halmashauri Kuu ya Taifa ilipitisha majina hayo na kuyakubali kuwa hao waliopendekezwa ndio hasa wanaofaa kuwa wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa.

 Mwenyekiti akawashukuru wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa waliopita na pia kuwataka wajumbe wapya kuchapa kazi, na kuwataka kujenga mustakabali wa Chama, Uimara na Umadhubuti kwa kufanya kazi kwa kushirikiana na kusaidiana.