Sunday, November 18, 2012

Mazungumzo na Malawi,Tanzania yasema ni karata ya Mwisho

Waziri Mambo ya Nje wa Tanzania Bernard Membe


SERIKALI ya Tanzania imesema kuwa itafanya mazungumzo ya mwisho na Malawi  kuhusu mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa, kabla ya kulifikisha suala hilo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ili kupatiwa ufumbuzi baada ya pande hizo mbili kushindwa kukubaliana.

Imesisitiza kuwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu, yaani Tanzania, Malawi na Msumbiji na hivyo siyo sahihi upande wowote kati ya nchi hizo kudai unamiliki sehemu kubwa ya ziwa.



Akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya kukutana na mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya nchini (EU) katika Ukumbi wa Karimjee Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe alisema kuwa tayari ujumbe kutoka Malawi umeshafika nchini kwa ajili ya mazungumzo hayo ambayo yamepangwa kufanyika kesho.

Waziri Membe alikutana na mabalozi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya kuwapa taarifa juu ya mambo yanayoendelea nchini zikiwamo vurugu za kidini zilizojitokeza hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Membe pia aliwaeleza wanadiplomasia hao kuhusiana na hali ya uhuru wa vyombo vya habari nchini, uamuzi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) kujihusisha mzozo unaoendelea huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa.

“Lakini pia nilikutana na mabalozi hao kuwaelezea hali ngumu ya uchumi wa nchi za ulaya na jinsi inavyoathiri maendeleo ya nchi za Afrika, “ alisema Waziri Membe na kuongeza kuwa:
“Timu ya Malawi ipo nchini kwa mazungumzo na keshokutwa (kesho) kutakuwa na mkutano wa mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizi mbili kuzungumzia chanzo cha mgogoro huu wa Ziwa Nyasa. Katika mkutano huo tutazungumzia tunakoelekea kwa kuwa tofauti zetu zipo wazi,” alisema Membe.

Alisema watakaoalikwa katika mkutano huo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Frederick Werema na Waziri wa Sheria, Mathias Chikawe na kwamba lengo la kuwaalika viongozi hao ni kutaka kulikabidhi suala hilo katika vyombo vya sheria.

“Baada ya mazungumzo tutasubiri baraka za Rais Jakaya Kikwete ambaye pia atashauriana na Rais wa Malawi, Joyce Banda ili kukubaliana suala hili liende ICJ,” alisema Membe.

Alisema kuwa  kabla ya kuchukua hatua hizo ni lazima wakutane na ujumbe huo kutoka Malawi.
“Timu ya Tanzania ambayo ipo makini inajipanga kwenda Umoja wa Ulaya,  Uingereza na Ujerumani kwa ajili ya kupata nyaraka zote za ushahidi na baada ya hapo utaanza mchakato wa kwenda ICJ,” alisisitiza.
Alisema kuwa mabalozi hao wamefurahia jinsi Tanzania inavyotatua mgogoro huo na Malawi kwa kutumia njia za kidiplomasia zaidi.

Source: Gazeti la Mwananchi

No comments: