Friday, December 14, 2012

ODM chamtetea Magufuli chasema hakuwakilisha CCM ni rafiki wa Odinga


Magufuli
Raila Odinga


Katibu Mkuu wa ODM, Profesa Peter Anyang’Nyong’ amesema hakuna haja ya Watanzania kumzonga Waziri John Magufuli, kwani ujio wake Kenya, ulitokana na mwaliko wa Odinga.

Profesa Anyang’Nyong’ ambaye chama chake cha ODM kilitangaza kuungana na chama kingine cha Wiper Democratic cha Makamu wa Rais, Kalonzo Musyoka katika uchaguzi huo alisema Odinga alimwalika Magufuli kama rafiki yake wa muda mrefu na rafiki wa ODM.
Raila Odinga na John Magufuli wakicheza pamoja Jukwaani

“Waziri Mkuu wetu Odinga ndiye aliyemwalika Magufuli na alimwalika kama rafiki yake wa karibu. Kuja kwake huku (Kenya) kulikuwa safari binafsi. Hakukuwa (kuja) na uhusiano wowote na wadhifa alio nao Tanzania,” alisema Profesa Onyang’Nyong’.

Alisema ziara ya Magufuli iliratibiwa na Odinga ambaye aligharimia kila kitu na kwamba mwaliko huo ulifanywa kwa kuzingatia ushirikiano wa muda mrefu baina yao.

Desemba 7 mwaka huu, chama hicho cha upinzani nchini Kenya kilimwalika Dk Magufuli kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika kwenye Uwanja vya Kasarani ambako pamoja na mambo mengine, alimpigia debe Raila Odinga ili achaguliwe kuwa Rais wa Kenya katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Machi mwakani.Hatua huiyo ilizua mjadala mzito ambapo Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kilidai ni makosa kwa Dk Magufuli kwenda Kenya na kutangaza kuumuunga mkono mmoja kati ya Wagombea wa urais nchini humo.

Kilisema ni makosa kwa nchi moja kuingilia siasa za nchi nyingine na kumtaka waziri huyo aeleze kama alitumwa na Serikali au la. 

Chadema pia kilimtaka Rais Jakaya Kikwete atolee kauli hatua hiyo ya waziri wake, vinginevyo nchi itakuwa na uhusiano mbaya na Kenya, endapo Raila hatachaguliwa kuwa Rais.

Hata hivyo Profesa Anyang’Nyong’ alisema ODM kumwalika Dk Mafuguli ni mwendelezo wa uhusiano wa wanasiasa wa Tanzania na Kenya uliokuwapo tangu enzi za viongozi; Jomo Kenyatta, Tom Mboya na Mwalimu Julius Nyerere ambao walifanya pamoja kazi ya kudai uhuru.

“Kizazi cha sasa lazima kitambue ushujaa wa viongozi wetu wa zamani ambao walituonyesha namna wanavyoweza kufanya siasa kwa pamoja na kufanikisha malengo yao,” alisema na kuongeza:

“Mambo kama haya lazima tuyatambue kwani sisi sote ni wamoja tena tuna shabaha ya kuwatumikia wananchi wetu. Tunapopata viongozi wenye mitazamo inayofanana kama ile ya waasisi wa mataifa yetu lazima tuwaunge mkono na kuwapa fursa.

“Kwetu sisi Magufuli tunamwona kama shujaa tena mtu ambaye anaweza kutoa idea (mawazo) yanayoweza kukusaidia kusonga mbele kwenye siasa.”
Alisema Dk Magufuli ana uzoefu mkubwa na mambo ya siasa na ODM wanatambua umuhimu wake katika siasa zao.

Alipuuza madai kwamba kumwalika Dk Magufuli ni kuingilia siasa za Kenya na huenda hatua hiyo ikadhoofisha uhusiano wa kidiplomasia… “ Kuja kwake hakumaanishi kwamba ameingilia mambo ya Kenya au siasa za taifa hili…. Huyu ni rafiki yetu na alikuwa kama mtu wetu wa karibu.”

“Nchi zetu zipo kwenye hatua ya kuwa na Serikali moja, wazo ambalo siyo geni sana kwetu maana hata waasisi wetu walikuwa na ndoto hiyo, hivyo kwa wakati huu kuwa na ushirikiano wa kisiasa ndani ya vyama vyetu ni jambo la muhimu kwani iko siku tutashuhudia tukiwa na Serikali moja.

Wakati ODM kikizungumzia suala hilo, baadhi ya viongozi wakuu wa Serikali wameshindwa kuzungumzia suala hilo baada ya kutupiana mpira.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema jana kwamba asingependa kuzungumzia suala hilo badala yake aandikiwe maswali na atayajibu wakati wowote… “Hili sizungumzi sasa. Niandikie maswali nitajibu.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira alimwagiza katibu wake aliyejitambulisha kwa jina la Joseph Lubiro kwamba suala hilo anayepaswa kulizungumzia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

“Nimeelezwa kwamba unahitaji kumwona Waziri anakwenda kwenye mkutano lakini nimemjulisha kile ulichokuwa unataka kujua na ameniambia kwamba nenda kwa Waziri wa Mambo ya Nje ndiye anayejua vyema safari zote za kikazi za viongozi wote wa Serikali,” alisema Lubiro.

Hata hivyo, habari zilizopatikana baadaye kutoka katika ofisi hiyo zilieleza kwamba hakuna rekodi yoyote inayoonyesha kwamba Dk Magufuli alikuwa na ziara ya kiserikali nchini Kenya.

.
  Source: Mwananchi

No comments: