Friday, December 28, 2012

Mengi yaibuka tukio la Padri kupigwa risasi Zanzibar

Padri Ambrose Mkenda
Kumekuwa na hisia tofauti kutoka kwa watu mbali mbali kufuatia Padri wa Kanisa Katoliki Zanzibar kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

PADRI Ambrose Mkenda alipigwa risasi wakati wa Siku kuu ya Kikristo ya Krismas Jumanne iliyopita, mjini Zanzibar na watu wasiojulikana

Hisia hizo zimezidi kuibua mengi ambapo wengi wametaka uchunguzi ufanyike na wahalifu wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Baadhi wamehusisha tukio hilo na kundi moja la kidini huko Zanzibar ambalo hivi karibuni lilisema lingewaua wachungaji na mapadri.Katika Sherehe za Krismas Umoja wa Makanisa ulitoa tamko ambalo pamoja na mambo mengine lilikemea uchochezi wa kidini  unaohamasisha kuwaua wachungaji na maaskofu.

Hata hivyo hadi sasa hakuna taarifa zozote zinazothibitisha kuwa kuna kundi lolote la kidini linahusika na tukio hilo.

Tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema inafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio la kupigwa risasi na watu wasiojulikana kwa Padri Mkenda.

Akizungumza na waandishi wa habari jana muda mfupi baada ya kumjulia hali Padri Mkenda, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Mohamed Aboud alisema Serikali inafanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tukio hilo.

Alisema kwa sasa ni mapema kujua chanzo cha tukio hilo kwani tayari vyombo vinavyohusika ikiwa ni pamoja na Jeshi la Polisi Zanzibar na Tanzania Bara vimeshapewa jukumu la kufanya uchunguzi.

“Tukio hili ni kubwa na limetuhuzunisha. Kwa kutambua umuhimu wa watumishi wa dini nchini, Serikali inafanya uchunguzi wa kina ili kutambua chanzo cha tukio hilo haraka,” alisema Aboud na kuongeza:
“Kwa sasa ni vyema tukawaachia madaktari ili wandelee na uchunguzi wa afya yake lakini ifahamike wazi kwamba Serikali ipo makini na pindi wahusika watakapopatikana watachukuliwa hatua kali za kisheria.”

“Nafahamu kwamba watu wanahisia tofauti lakini nataka mfahamu kwamba sisi kama Serikali hatuwezi kusema chochote kuhusiana na tukio hili kwani bado tunafanya uchunguzi ili kuwabaini wahusika.”
Mkuu wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi Tanzania, (SACP), Simon Siro ambaye pia alimtembelea Padri huyo jana alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na kuahidi kwamba wahusika watakamatwa.

“Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi. Wote waliohusika watakamatwa na kushughulikiwa kwani kitendo hicho siyo cha kibinadamu,” alisema Siro.

Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Jumaa Almasi alisema hali ya Padri Mkenda inaendelea vizuri na kwamba madaktari wanaendelea kumfanyia uchunguzi pamoja na kumpa matibabu.

Tukio la kupigwa risasi kwa padri wa Kanisa hilo ni lapilli baada ya Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soraga kumwagiwa tindikali usoni na kifuani na watu wasiojulikana.

No comments: