Sunday, January 6, 2013

Maiti Zaidi ajali ya boti Ziwa Tanganyika, 21 wafa maji

Deutsch: Der Tanganjikasee bei Kigoma, Langzei...
Ziwa Tanganyika

Juhudi za ukoaji zinaendelea katika ziwa Tanganganyika ambapo watu 21 wanasadikiwa kufa maji kufuatia boti waliyokuwa wakisafiria kutoka Kijiji cha Kirando wilayani Nkasi, kuelekea Rumonge nchini Burundi, kupasuka na kuzama katika Kijiji cha Herembe.

Kwa mujibu wa nahodha bot hiyo ambaye amenusurika maiti tisa ndizo zilizopatikana, huku maiti kumi na mbili zikiwa hazijulikani zilipo ziwani humo.

Abiria walionusurika wanasema , chanzo cha ajali hiyo ni upepo mkali uliotokea katika eneo hilo la Herembe na kusababisha mashine ya boti hiyo kushindwa kufanya kazi.Boti hiyo inayojulikana kwa jina la Yarabi Salama, ilikuwa na abiria wanaokadiriwa kufikia 85, ambapo abiria 65 waliokolewa huku wengine 21 wakihofiwa kupoteza maisha.

Kutokana na tatizo hilo, boti hiyo ililegea na kuvunjika jambo lililosababisha boti hiyo kujaa maji na kuzama ziwani pamoja na abiria.

Boti hiyo ilibeba shehena kubwa ya abiria na mizigo tani 45 za mihogo, dagaa na samaki zikisafirishwa kuelekea Rumonge nchini Burundi.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Serekali ya Kijiji cha Herembe, Joka Mpapi na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Adam Makuka, wamelalamikia ukosefu wa vifaa vya uokoaji.

Naye  Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Mstaafu Issa Machibya, aliwataka wananchi kuwa makini na usafiri wa majini na pia wachukue tahadhari ya kupakia mizigo.

Kanali Machibya alisema Serikali itaendelea kutoa msaada kwa wafiwa, huku akiwataka watumishi wa vyombo hivyo kubeba abiria na mizigo kulingana na uwezo wa chombo.

“Hivi sasa kuna mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa hivi sasa imebadilika sana ndugu zangu, lazima mchukue tahadhari mnaposafirisha bidhaa zenu mbebe abiria na mizigo kulingana na uwezo wa boti husika,” alisema Machibya.

Maiti zote zilizopatikana katika eneo la ajali zimehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa Maweni.