Saturday, January 5, 2013

Membe, Lowasa sasa hapatoshi Urais 2015: Membe Aaga Ubunge

Ikulu ya Tanzania
Vita vikali vya kuwania Urais vimeanza nchini Tanzania ambapo Wanasiasa tayari wameanza kutangaza au kuonyesha kila dalili kuwa sasa wameanza harakati za kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi nchini Tanzania.

Benard Membe
Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe tayari ametangaza rasmi kuwa hatogomea tena ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.

Membe ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mtama, mkoani Lindi, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza kwenye sherehe za Mwaka Mpya nyumbani kwake.
“Unajua nimekuwa mbunge wenu kwa kipindi cha tatu. Hivi leo ninawaaga rasmi kuwa sitagombea tena nafsi hii ya ubunge,” alisema Membe.

Kauli hiyo ya Membe inatafsiriwa na wataalamu wa masuala ya siasa kuwa huenda ameamua kufanya hivyo ili aweze kugombea urais mwaka 2015. Membe ni mmoja kati ya watu wanaolezwa kuwa ana mpango huo wa kutaka kuchukua madaraka hayo makubwa nchini Tanzania.

Mwingine anayetajwa kuwania nafasi hiyo ni Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa ambapo juma hili vyombo vya habari vya Tanzania vilimnukuuu Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo akitangaza kuchukua kile alichokiita uamuzi mgumu ili kuhakikisha kuwa Mbunge wa Monduli (CCM), Edward Lowassa anamrithi Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Edward Lowassa



Shelukindo alitoa kauli hiyo Jumapili wakati akiwasalimia wakazi wa Monduli baada ya kukaribishwa kuchangia ujenzi wa Hosteli ya KKKT katika sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zilizofanyika nyumbani kwa Lowassa ambazo pia zilihudhuriwa na makada kadhaa wa CCM.

Jana alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Shelukindo alisema: “Ni kweli mimi ni muumini wa Lowassa, ila pale (mkutanoni) sikumtaja kwa sababu najua chama kina taratibu zake na muda wa mchakato wa kumpata Rais haujafika.”
“Niliposimama niliwaeleza kuwa nisingeweza kuchangia fedha nyingi kwa sababu watu wangu wana njaa huko Kilindi. Pia kule (Kilindi) tunaendesha harambee ya aina hiyohiyo. Ila nikawaambia zawadi yangu kwa Wanamonduli ni kufanya uamuzi mgumu ili mwaka 2015 apatikane Rais mzalendo na anayeweza kufanya uamuzi mgumu na kwa wakati.”

Shelukindo aliendelea: “Niliposema hivyo, umati uliibuka kwa shangwe na kunitaka nimtaje nitakayeshirikiana naye, lakini nikawaambia kuwa huu si wakati mwafaka ila baadaye nilichangia Sh500,000.”