Tuesday, January 15, 2013

Wawili wazikwa hai na maiti, Wafariki wakiwa kaburini

WAKAZI wawili wa Kijiji cha Karungu, Kata ya Ivuna, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa wakiwa hai katika kaburi moja na marehemu wanaodaiwa kumuua, tukio linalohusishwa na imani za kishirikina.

Watu hao, Ernest Molela anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 60 na Bibi Mizinala Nachela ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 50, walizikwa wakiwa hai pamoja na aliyekuwa mkazi wa kijiji hicho, marehemu Nongwa Hussein.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba aliema kuwa, tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa tano na sita mchana, muda mfupi kabla ya maziko ya Hussein.Kabla ya kufukiwa katika kaburi moja na marehemu, Molela na Nachela kwa nyakati tofauti walipigwa hadi kuzirai na watu wanaodaiwa kushiriki kuchimba kaburi kwa ajili ya kumzika marehemu Hussein.

Silwimba alisema Hussein alifariki dunia Jumamosi saa 10 jioni baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini inaonekana kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walihusisha ugonjwa huo ambao ulisababisha kifo chake na ushirikina.

Jana mchana, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Momba aliyefahamika kwa jina la Wendo aliongoza operesheni ya kufukua kaburi walimozikwa watu hao, ambao walikutwa wakiwa wameshafariki dunia.

Silwimba alisema miili ya Molela na Nachela ilifanyiwa uchunguzi, kisha kukabidhiwa kwa ndugu na jamaa zao ambao waliifanyia mazishi jana mchana.

Mkasa wenyewe
 Kundi la vijana tisa ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliokuwa wakichimba kaburi la marehemu Hussein walianza msako katika Kijiji cha Karungu wakiwatafuta wale waliowatuhumu kwamba ni wachawi na kwamba walihusika na kifo chake.

Silwimba alisema katika harakati zao, walikwenda nyumbani kwa George Hussein ambaye ni kaka wa marehemu lakini hawakumkuta, hivyo kuamua kuchoma moto nyumba yake kwa kuwa walikuwa wakimtuhumu kuhusika na kifo hicho.

“Baada ya kufanya uharibifu huo, walikwenda hadi nyumbani kwa Mzee Molela kisha wakamkamata na kumpiga sana hadi hali yake ikawa mbaya kisha wakambeba hadi eneo la maziko,” alisema na kuongeza:

“Waliporejea kwenye msiba walimkuta Mama Nachela naye wakamkamata na kuanza kumpiga hadi akazimia na yeye pamoja na Molela waliwavuta hadi kwenye kaburi ambako mazishi ya Nongwa (Hussein) yalifanyika.”

Alisema baada ya jeneza kushushwa kaburini, vijana hao wanaodaiwa kwamba walikuwa na hasira walimvuta Molela na kumwamuru kuweka udongo kaburini, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na hali yake kuwa mbaya.

“Baada ya kushindwa walimsukumiza kaburini na baadaye walimvuta yule mama (Nachela) ambaye naye alikuwa hajitambui na kumtupa ndani ya kaburi halafu wakawafukia wote, kisha wakaondoka,” alisema Kaimu Ofisa Mtendaji huyo.

Alisema mwingine aliyekuwa akisakwa na vijana hao ni Fotino Sichilongwa na kwamba kabla ya kufanya vitendo hivyo, vijana hao walimkamata Mwenyekiti wa Kitongoji, Alfred Kukwe na kumfunga miguu na mikono kwa kutumia kamba, wakamlaza kifudifudi, kisha kumnyang’anya simu yake ya kiganjani ili asiweze kutoa taarifa kokote.

Alisema Kukwe alifunguliwa kamba hizo saa saba na nusu mchana na ndipo alipopiga simu sehemu mbalimbali kutoa taarifa za tukio hilo.

Silwimba alisema baada ya taarifa hizo kusambaa kijijini Karungu, mwenyekiti wa kijiji hicho na ofisa mtendaji wake, walikimbia na kwenda kujificha kusikojulikana wakihofia kudhuriwa na vijana hao.

“Polisi walipofika jana (juzi) jioni walikuta vijana wote waliohusika wamekimbia na hawajulikani walipo maana nyumba zao zimefungwa, hili ni tatizo kubwa maana limesababisha taharuki kubwa hapa kijijini,” alisema.

Wawili mbaroni
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kulikuwa na taarifa kuwa Molela na Nachela wana undugu. Hata hivyo, habari kutoka kijijini Karungu zimesema hawana undugu wowote.

Kamanda Diwani ambaye aliwashutumu wananchi kwa kujichukulia sheria mkononi, alisema hadi sasa watu wawili wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.“Tunawashikilia watu wawili ambao tunaamini walikuwa vinara wa tukio hili la mauaji,” alisema Diwani.
Kamanda huyo aliitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake waheshimu na kutii sheria bila shuruti na kuachana na imani za kishirikina.

“Kila mmoja afanye mambo yake kwa kujiamini. Hii ya kuendekeza imani za kishirikina ina madhara na zaidi ni kurudisha nyuma maendeleo. Jamii inatakiwa kutafuta njia halali kufikisha kero na malalamiko badala ya kutumia vurugu na fujo na kusababisha mauaji.”

Source:Mwananchi

No comments: