Monday, February 25, 2013

Maalim Seif apinga mauaji ya Padri asema si ya kigaidi


Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amepinga kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi kuwa mauaji ya viongozi wa dini Zanzibar ni ugaidi na kusema kuwa wanaofanya hivyo ni watu wenye nia ya kuvunja umoja wa Wazanzibari.

Baada ya mauaji ya Padre Evarist Mushi, akizungumza na wandishi wa habari,Nchimbi alielezea kusikitishwa na mauaji hayo akisema kuwa ni ya kigaidi na yana lengo la kuingiza nchi katika machafuko. Amesema kuwa tukio hilo si tukio la ujambazi bali tukio la kigaidi kwani limelenga zaidi katika kuwashambulia viongozi kidini.


Padre Evaristus Mushi aliuawa Februari 17, mwaka huu kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana waliokuwa katika pikipiki aina ya Vespa wakati akienda kuongoza misa katika Kanisa la Mtakatifu Theresia la Beit el Rass.

“Watu hawa wameamua kuyatumia matukio ya kuuawa na kujeruhiwa kwa viongozi wa kidini ili kuvunja umoja wa Wazanzibari, lakini nasema hakuna ugaidi Zanzibar,” alisema Maalim Seif juzi usiku alipohutubia kwenye hafla ya Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) mjini Kiuyu, Wilaya ya Wete, Kaskazini Pemba.

Alisema hivi sasa Wazanzibari ni wamoja na watu hao wenye nia mbaya wanayachukulia matukio hayo kwa kutaka kuwagawa na kuwaletea mtafaruku kwa kuonyesha kuwa kuna tofauti za kidini Zanzibar wakati siyo kweli.

Alisema inasikitisha kuona wapo baadhi ya viongozi wenye nia chafu dhidi ya Zanzibar wenye tabia ya kutoa kauli za kujenga chuki na fitina miongoni mwa Wazanzibari chini ya kivuli cha matukio hayo.

Makamu huyo wa Kwanza wa Rais alisema, kinachoonekana kuna ajenda imetayarishwa ya kutaka kulazimisha chuki za kidini Zanzibar, licha ya kuwapo kwa historia ya miaka mingi ya watu kuvumiliana na kuishi kwa pamoja na kuwapo watu wa imani tafauti.

Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar hivi sasa kuwa macho na ajenda zinazolengwa kuwavuruga na waendelee kuishi kwa mshikamano na umoja kama ambavyo wamekuwa wakiishi.

Maalim Seif alisema vitendo vya kuuawa na kujeruhiwa viongozi wa kidini Zanzibar ni mambo mageni na kwa miaka mingi Zanzibar imekuwa ni mfano bora wa uvumilivu wa kiitikadi za kidini, licha ya kuwa asilimia 98 ya wananchi wake ni Waislamu.

Alisema Katiba ya Zanzibar imeweka wazi haki ya mtu kuabudu kwa mujibu wa imani yake na uhuru wa mtu kuabudu umelindwa.

“Ni Sultani wa Zanzibar ambaye alikuwa Muislamu ndiye aliyetoa ardhi kwa Wakiristo kujenga Kanisa. Juzi nilipokwenda kutoa salamu za rambirambi kwa Baba Askofu Shayo, baada ya kifo cha Padri Mushi, aliweka bayana kuwa lililotokea lisihusishwe na tofauti za kidini,” alisema Maalim Seif.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema inasikitisha kuona wakati Rais Jakaya Kikwete katoa maelekezo uchunguzi wa kina ufanyike na Kamishna wa Polisi Zanzibar ameshaweka wazi kuwa uchunguzi unaendelea, baadhi ya viongozi na vyombo vya habari vinachochea chuki za kidini na kusema kuwa Zanzibar kuna ugaidi.

Aliwataka wananchi wote wa Zanzibar kwa wakati huu kuwa watulivu na wasitawaliwe na jazba na wala wasichokozane, pia wasikubali kuchokozeka.


Akizungumzia matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotolewa hivi karibuni, Makamu wa wa Kwanza wa Rais alisema ni matokeo mabaya na ya kuliza, kwa sababu hayaonyeshi mustakabali mwema kwa watoto wetu na nchi yetu hapo baadaye.


Alisema ni wakati mwafaka Serikali, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, walimu na jamii nzima kujiuliza nini sababu ya matokeo hayo mabaya, na kujiuliza pia nchi inaelekea wapi?

Maalim Seif alisema sasa si wakati tena wa kutupiana lawama, lazima pande zote zikae zijadili wapi pamekosewa, ili ufumbuzi uweze kupatikana na hali kama hiyo isitokee tena siku nyingine.

Source: Mwananchi

No comments: