Monday, February 4, 2013

Vurugu Kubwa CCM,CHADEMA wazichapa damu yamwagika

Wafuasi wa CCM wakimtimua kwa mawe mfuasi wa CHADEMA wakati wa vurugu hizo
Vurugu kubwa imetokea mkoani Dodoma kati ya wafuasi wa chama  cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA na wale wa CCM  wakati wakigombea eneo na mti wa kutundika bendera za vyama vyao ambapo inasemekana watu kadhaa wamejeruhiwa..

Vurugu hizo zilizotulizwa na Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), zilitokea jana mchana katika uwanja huo uliopo karibu na Baa ya Mwanga, baada ya CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwepo uwanjani hapo, ili waweke bendera zao kwa ajili ya mkutano ambao ulikuwa sehemu ya maadhimisho hayo.Vurugu zilizuka baada ya wafuasi wa Chadema kuwataka wenzao wa CCM waendelee na mkutano katika eneo hilo kwa sharti la kurejeshwa kwa bendera iliyong’olewa. Wafuasi wa vyama hivyo wakiwamo wabunge wa CCM walionekana wakivutana kunyang’anyana mti wa bendera.
“Baada ya CCM kugoma, Chadema walijaribu kurudisha bendera hiyo kwa nguvu, jambo ambalo lilifanya wafuasi wa CCM waanze kuokota mawe na kuwarushia wapinzani wao hao, huku Chadema nao walianza kujibu mapigo,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Baadhi ya wabunge wa CCM walioshiriki katika vurugu hizo na majimbo yao kwenye mabano ni Ismail Aden Rage (Tabora Mjini), Nyambari Nyangwine (Tarime), Seleman Jafo (Kisarawe), Said Mtanda (Mchinga) na Mary Chatanda (Viti Maalumu).

Baadhi ya wafuasi wa CCM walionekana wakibeba mawe na kuwapiga wenzao wa Chadema na kusababisha tafrani kubwa katika eneo hilo la mkutano.

Katibu wa Chadema Wilaya ya Dodoma Mjini, Jellah Mambo alisema kuwa tukio hilo limetokana na wafuasi wa CCM kung’oa bendera ya Chadema iliyokuwa ikipepea eneo la Mwanga Baa kulikofanyika sherehe za chama chao (CCM).
“Kwanza wamechukua bendera yetu. Halafu tumeshangazwa na CCM kuruhusiwa kufanya maadhimisho yao wakati kuna agizo la Mkuu wa Mkoa na polisi kukataza mikusanyiko ya kisiasa wakati wa Bunge.
“Kwa nini sisi (Chadema) tuzuiwe mikutano yetu wakati wenzetu wanafanya? Huku si kutenda haki....Tulikuwa na mikutano ya kuimarisha chama katika kata kuanzia Ijumaa, Jumamosi na Jumapili, lakini tumezuiwa na tukaheshimu mamlaka,” alisema katibu huyo.

Pia tulikuwa tufanye mkutano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma, lakini tukazuiwa na tuliheshimu amri hiyo, alisema.

Mambo alisema katika vurugu hizo wafuasi wawili wa Chadema; Idd Kizota na Anord Swai waliumizwa na kushonwa nyuzi saba usoni.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Ezekiel Mpuya alisema hana taarifa za majeruhi hao.

“Ni vigumu kujua, unless (isipokuwa) wafike hospitalini wakisindikizwa na kundi la wafuasi wenzao waliokuwa kwenye sare. Kama walikuja kama wagonjwa wengine sio rahisi sana kwangu kujua,” alisema Dk Mpuya.

Kumi mbaroni
Vurugu hizo zilizosababisha watu wawili kuumizwa vibaya, zililazimisha Jeshi la Polisi kuwatia mbaroni watu kumi wanaosadikiwa kuwa wafuasi wa Chadema

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alikiri kutokea vurugu hizo, lakini akasema bado anafanyia kazi suala hilo.

Kamanda Misime alikiri Serikali mkoani Dodoma kuzuia mikutano ya kisiasa wakati wa Bunge, lakini akasema kwa CCM ni tofauti kwa kuwa hizo ni sherehe zao za kuzaliwa kwa chama.
“Ninasoma hapa magazeti yenu, mmeandika wenyewe maadhimisho ya miaka 36. Sasa hawa wanaadhimisha hiyo miaka 36 na siyo mkutano wa kisiasa...Tulichokataza ni maandamano, misafara ya pikipiki na kufanya mikutano ya siasa,” alisema Misime.

Akihutubia katika mkutano huo baada ya hali kutulia mgeni rasmi, Mbunge wa Jimbo la Tarime, Nyangwine aliwakandia wapinzani na kusema kuwa wanachokifanya ni kuendeleza vurugu nchini na hawana sera ya maendeleo.
“Hivi jamani, hii leo hawa jamaa watasema nini? Kama suala la barabara, leo hii unaweza kutoka Mtwara hadi Mwanza kwa baiskeli, kama maji, michakato inafanyika, kama umeme ndiyo usiseme, hivi wanataka nini?
“Hawa jamaa wamezoea kufanya vurugu...Si mmeona wenyewe hapa, hawana lolote zaidi ya kufikiria vuru, wananchi msikubali kuhadaiwa,”alisema.

JK akemea mifarakano
Akizungumza mkoani Kigoma kulikofanyika maadhimisho hayo kitaifa, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alikemea siasa za makundi ndani ya chama, akisema tabia hiyo haijengi.

“Mifarakano ndani ya chama inayopaliliwa na viongozi ndani ya chama, inakibomoa chama na ndiyo maana tumepoteza majimbo matano katika uchaguzi uliopita,” alisema.

Source: Habari na Picha kwa hisani ya Mwananchi

No comments: