Monday, April 29, 2013

Lema leo kutinga mahakamani, Arusha hofu yatanda


Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema leo asubuhi anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.


Lema aliyekamatwa usiku wa manane kuamkia Ijumaa wiki hii, alihojiwa kwa saa tatu mfululizo katika Kituo Kikuu cha Polisi, Arusha lakini alinyimwa dhamana kwa maelezo kwamba kuachiwa kwake kungehatarisha amani.

Wakili wa Lema, Humphrey Mtui alisema mahojiano ya mteja wake na polisi yalidumu kwa zaidi ya saa tatu kuanzia saa 7:50 mchana hadi saa 11:15 jioni, na kwamba walitaka ufafanuzi kwenye hoja tatu walizodai kwamba zilijengwa kwenye kauli alizotoa Lema wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA).
Maneno hayo yanayotafsiriwa na polisi kuwa ni uchochezi ni pamoja na “Dhambi mbaya na kubwa kuliko zote duniani ni woga” na “Nimepata taarifa kuwa ndani ya dakika 15 Mkuu wa Mkoa atafika, asipofika ndani ya muda huo nitawaongoza kwenda kudai haki yenu ya msingi ya kupatiwa ulinzi.”
Kauli nyingine ni “Hawa ndio viongozi wetu (akimaanisha mkuu wa mkoa), tunaowategemea wanakuja kwenye matatizo wakijivuta utafikiri wanakwenda kwenye send-off.”
Lema anadaiwa kutamka maneno hayo baada ya Mulongo kugoma kuzungumza na wanafunzi kisha kurejea ndani ya gari akitaka viwepo vipaza sauti, kitendo kilichowafanya wanafunzi kuanza kumzomea kabla polisi kuanza kulipua mabomu ya machozi na kumwondoa eneo la tukio mkuu huyo wa mkoa.
Lema na Mulongo wote walikwenda IAA kutokana na tukio la kuuawa kwa kuchomwa kisu kwa aliyekuwa mwanafunzi wa taasisi hiyo, Henry Kago.
Baada ya vurugu hizo Mulungo alimtuhumu Lema kuandaa mazingira ya yeye kuzomewa .