Sunday, April 14, 2013

Mwandishi mbaroni kwa kuhusishwa kutekwa kwa Kibanda

Majid Mjengwa
Absalomu Kibanda muda mfupi baada ya kutekwa na kuteswa

Kuna taarifa kuwa Mwandishi wa safu katika magazeti mbalimbali nchini, Majid Mjengwa amekamatwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda.

Habari zilizopatikana jijini Dar es Salaam na baadaye kuthibitishwa na polisi zinasema Mjengwa alikamatwa muda wa asubuhi na kwamba alikuwa akihojiwa na makachero wa jeshi hilo hadi alasiri kuhusu tukio la kuteswa kwa Kibanda.

Msemaji Mkuu wa Polisi Advera Senso aliliambia  gazeti la Mwananchi kwamba:
“Ni kweli kwamba tunaye, tunaendelea kumhoji, tunachoomba ni kwamba mtupe nafasi ili tufanye kazi yetu na kukiwa na jambo lolote tutawajulisha.”


Hata hivyo, Senso hakuwa tayari kueleza kwa undani muda aliokamatwa Mjengwa wala sababu za kukamatwa na kuhojiwa kwake, lakini chanzo chetu ndani ya Jeshi la Polisi kilithibitisha kwamba pamoja na mambo mengine kuhojiwa kwake kulihusu uteswaji wa Kibanda.

Jumatatu wiki hii, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Nchini, Issaya Mngulu alisikika akizungumza na Kituo cha Radio One cha Dar es Salaam kwamba kesho Jumatatu (April 15, 2013) polisi watatoa taarifa rasmi ya hatua waliofikia katika upepelezi wa kesi ya Kibanda.

Kwa upande wake Mia Mjengwa ambaye ni mke wa Mjengwa, alisema mumewe alipata wito kutoka polisi makao makuu Alhamisi na kwamba juzi Ijumaa alisafiri kutoka Iringa kwenda Dar es Salaam kuitikia wito huo.
“Ninachojua ni kwamba aliitwa kwenda polisi na leo (jana) alinipigia simu kama saa 7:00 mchana na aliniarifu kwamba yupo polisi, sasa tangu wakati huo sijaongea naye tena na wala simu zake hazipatikani,” alisema Mia na kuongeza: “Kwa hiyo mimi kwa kweli sifahamu kwamba anahojiwa kwa sababu gani.”

Taarifa za kukamatwa kisha kuhojiwa kwa Mjengwa ambaye pia ni mmiliki wa Mjengwa Blog, zimekuja siku chache tangu msaidizi wake katika Blog hiyo, Joseph Ludovick akamatwe, kuhojiwa kisha kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi.

Ludovick alifikishwa mahakamani pamoja na Mkurugenzi wa Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Willifred Lwakatare wakikabiliwa na tuhuma za ugaidi na kupanga kumteka Mhariri Mtendaji wa Mwananchi, Dennis Msacky.

Kuteswa Kibanda
Machi 5, mwaka huu saa 5.30 usiku, Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alinusurika kifo baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kisha kupigwa na kujeruhiwa vibaya.

Kutokana na shambulio hilo, Kibanda alikimbizwa nchini Afrika Kusini ambako alipewa matibabu, lakini madaktari bingwa katika hospitali ya Milpark walishindwa kuliokoa jicho lake la kushoto ambalo liliharibiwa vibaya na watesaji wake. Jicho hilo liling’olewa na sasa anasubiri kuwekewa la bandia.

Mbali na kupoteza jicho, Kibanda pia alijeruhiwa kichwani ambako alipata majeraha makubwa mawili na kushonwa nyuzi kadhaa, kuvunjwa meno mawili na kung’olewa kucha katika moja ya vidole vyake vya mkono wa kushoto, pia kujeruhiwa katika mguu wake wa kushoto.

Tukio hilo lilifananishwa na lile la kutekwa, kuteswa, kuumizwa vibaya, kung’olewa meno na kucha na kisha kutelekezwa katika Msitu wa Pande kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Stephen Ulimboka lililotokea usiku wa Juni 26, mwaka jana.

Kibanda alishambuliwa na watu ambao walivamia gari lake wakati akisubiri kufunguliwa kwa lango la kuingia nyumbani kwake Mbezi Juu na alipojaribu kuwakimbia alianguka hivyo walipata nafasi ya kumshambulia kiasi cha kupoteza fahamu.
Polisi walitangaza kuunda jopo la wapelelezi kumi waliobobea katika masuala ya upelelezi.

Source: Mwananchi

No comments: