Monday, April 15, 2013

Waandishi wengine wahojiwa na Polisi kuhusu vurugu Mtwara


Baada ya mwandishi wa habari Majid Mjengwa kutiwa mbaroni na polisi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na tukio la kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Waandishi wa habari wengine wamehojiwa kutokana na sakata la vurugu za gesi Mtwara wakidaiwa kuhusika na uchochezi uliosababisha vurugu hizo.


Vurugu hizo zilitokea Januari 26, mwaka huu na kuendelea kwa nyakati tofauti hata kusababisha nyumba za baadhi ya wabunge, viongozi wa CCM, Mahakama na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi pamoja na magari 18 na pikipiki saba kuteketezwa kwa moto na wananchi ambao walidaiwa kupinga mpango wa Serikali kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mtwara (MPC), Hassan Simba alithibitisha kuhojiwa kwa waandishi wa habari kuhusiana na sakata hilo.

Waandishi waliohojiwa hadi jana jioni ni Andrew Mtuli (Redio Pride FM), anayedaiwa kuendesha kipindi cha Amka na Pride kinachorushwa na redio hiyo kila alfajiri wakati Emmanuel Msigwa ambaye ni mtangazaji wa vipindi mbalimbali, Hassad Mdimu mtangazaji wa Kipindi cha Joto la Wiki ambaye anatuhumiwa kuweka hotuba ya kiongozi mmoja iliyoitwa ya uchochezi, wote wakiwa ni watangazaji wa kituo hicho cha redio.

Ilielezwa kuwa mahojiano hayo yanafanywa na makachero wa polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam na kwamba mbali na waandishi wa habari pia imeelezwa watu wa kawaida wamehojiwa na wengine wanaendelea kuhojiwa kuhusiana na vurugu hizo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki hakuweza kupatikana jana katika simu yake kutokana na kudaiwa kuwa katika pilikapilika za uhamisho kutokana na Inspekta Jejenrali wa Polisi (IGP) Said Mwema kufanya mabadiliko kwa baadhi ya Makamanda wa Polisi kwa Mikoa ya Singida na Mtwara.

Wakati huohuo, mwandishi wa habari wa vyombo mbalimbali Majid Mjengwa ataendelea kuhojiwa na polisi Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam leo asubuhi.

No comments: