Thursday, May 23, 2013

Kikwete awaka vurugu za Mtwara
Rais Jakaya Kikwete amekemea vikali vurugu zilizotokea jana mkoani Mtwara baada ya kusomwa bungeni kwa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Akizungumza katika eneo la Kizota, Dodoma wakati wa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Barabara ya Dodoma kwenda Iringa, Rais Kikwete alisema wote waliohusika na vurugu hizo watasakwa na kuchukuliwa hatua kali.
Rais Kikwete alisema rasilimali inayopatikana mahali popote pale nchini inatakiwa kutumiwa na Watanzania wote... “Hivi watu wa Nyarugusu wadai dhahabu ya pale au kinachopatikana Chalinze basi kisitumiwe na watu wa Morogoro! Hivi tutakuwa na taifa kweli?,” alihoji kwa ukali Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisisitiza kuwa Serikali itawasaka wale wote wanaoongoza vurugu hizo na watawajibishwa kwa makosa hayo... “Tutawasaka hawa watu na viongozi wao hata kama wana mapembe kiasi gani, tutayakata.”
Alichosema Waziri Muhongo
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amesema mradi wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda Dar es Salaam, umeanza kwa kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakwenda huko wiki ijayo kuweka jiwe la msingi.
Akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini jana, Waziri Muhongo alisema:
“Mradi wa kujenga bomba la gesi uko palepale na unaendelea kwa kasi na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ataenda kuweka jiwe la msingi wiki lijalo.”
“Tumezungumza mengi kuhusu suala hilo na hata viongozi wa watu wa Mtwara walipelekwa nje kujifunza faida zake, lakini hata kama hawajaelewa, nimetoa kijitabu kinachozungumzia faida mbalimbali watakazopata wana Mtwara katika mradi huo.”
Profesa aliyeanza hotuba yake kwa kueleza machapisho mbalimbali yaliyotolewa na wizara yake kufafanua faida za gesi ya Mtwara kwa taifa, alisema mradi huo uliozinduliwa Novemba mwaka jana na Rais Kikwete, unahusisha ujenzi wa bomba lenye urefu wa kilometa 532 na kipenyo cha nchi 36.
“Bomba hilo lina uwezo wa kusafirisha futi za ujazo za gesi milioni 784 kwa siku. Mradi utahusisha mitambo miwili ya kusafirisha gesi asilia katika maeneo ya Mnazi Bay- Madimba (Mtwara) na Kisiwa cha Songosongo (Lindi). Utagharimu Dola za Marekani 1,225.3 milioni,” alisema.
Alisema kazi za usanifu wa mradi na ulipaji fidia kwa wananchi wapatao 3,092 waliopisha maeneo ya mradi, zimekamilika na hatua za awali za ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi asilia zimeanza.

No comments: