Thursday, May 9, 2013

Lwakatare kidedea, afutiwa mashtaka ya Ugaidi


Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewafutia mashtaka matatu ya ugaidi, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura.

Mashtaka yaliyofutwa ni ya pili, tatu na nne. Shtaka la kwanza ambalo ni la kawaida la jinai limebaki. Yaliyofutwa ni kupanga njama za utekaji nyara dhidi ya Dennis Msacky kinyume na Kifungu cha 21 cha sheria inayopinga ugaidi. 

Shtaka la tatu ni walipanga na kushiriki katika mkutano wa kupanga kitendo cha ugaidi cha utekaji nyara dhidi ya Msacky na la nne ni lilikuwa likimkabili Lwakatare la kuhamasisha vitendo vya kigaidi.

Katika shtaka la kwanza ambalo ndilo lililobaki, washtakiwa hao wanadaiwa kula njama kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu kinyume na Kifungu cha 227 cha Sheria ya Kanuni ya 
Adhabu.

Kwa uamuzi huo, washtakiwa hao wanaweza kuomba dhamana wakati kesi yao itakapotajwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 13, mwaka huu.

Katika uamuzi wake, Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu alikubaliana na hoja za mawakili wa Lwakatare kuwa mashtaka hayo hayana maelezo ya kutosha kuonyesha kuwa ni ya ugaidi akisema yalipaswa yawe na maelezo yanayoelezea uhalisia wa ugaidi.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi ya mawakili wa watuhumiwa hao kupinga uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa kuwafutia kesi na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi yenye mashtaka hayohayo kwenye Mahakama ya Kisutu, Machi 20, mwaka huu.

Jaji Kaduri alikubaliana na hoja za Wakili wa Serikali, Prudence Rweyongeza alizozitoa wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kuwa uamuzi wa DPP ulikuwa sahihi.
Lwakatare na Rwezaura walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Machi 18 na kusomewa mashtaka hayo manne katika kesi namba 37 ya mwaka 2013.