Saturday, May 25, 2013

Vurugu Mtwara:vigogo serikalini Mtwara kikaangoni





Wabunge wa CCM wamekuja juu na kumtaka Rais Jakaya Kikwete kuwafukuza kazi vigogo wa Serikali mkoani Mtwara, wakiwamo Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kutokana na kile walichoeleza ni uzembe uliochangia vurugu zinazoendelea za wananchi kugomea gesi kutoka nje ya mkoa huo.
Wengine waliopendekezwa kuchukuliwa hatua ni kamati nzima ya ulinzi na usalama ya ngazi ya mkoa na wilaya ya Mtwara mjini, wakiwamo makamanda wa polisi.
Kutokana na hali hiyo, vigogo kadhaa mkoani humo wako hatarini kukumbwa na ghadhabu hiyo akiwamo Mkuu wa vikosi vya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mkuu wa mgambo na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wabunge hao walikuwa wakitoa mapendekezo hayo kwenye kikao cha Kamati ya Wabunge wa CCM iliyofanya kikao cha dharura juzi usiku, mjini hapa.
Kikao hicho kiliongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, huku Spika wa Bunge, Anne Makinda ambaye wakati huo alikuwa kwenye kikao cha Kamati ya Uongozi wa Bunge, aliwakilishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Jenista Mhagama.
Katika kikao hicho maalumu kilichokusudia kutoa ushauri kwa Rais Kikwete juu ya njia mwafaka ya kutatua hali ya machafuko, wabunge wengi wali kukasirishwa na jinsi hali ilivyo mkoani Mtwara. Chanzo chetu kwenye kikao hicho kilieleza kuwa wabunge hao walichukizwa na jinsi Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya walivyokuwa wakipingana kimsimamo. Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Joseph Simbakalila, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Wilman Ndile na Kamanda wa Polisi Mkoa Linus Sinzumwa wamehusishwa.
Licha ya baadaye kuonekana kuwa kitu kimoja, wabunge hao walidai kuwa walishindwa kutumia nafasi zao katika kutatua tatizo hilo, ambalo hadi juzi Serikali ilisema walikuwa wamekufa watu watano, wakiwamo wanajeshi wa JWTZ waliofariki katika ajali wakati wakienda kutuliza machafuko.
Chanzo hicho kilieleza kuwa iwapo mapendekezo ya wabunge hao yatapelekwa kwa Rais Kikwete kama michango ya wabunge hao ilivyokuwa, huenda rungu likawaangukia pia viongozi wa kisiasa wa CCM mkoani humo. Miongoni mwa wanasiasa hao, chanzo hicho kimesema ni wale waliotoa kauli za waziwazi kuunga mkono msimamo wa kutoruhusu gesi kusafirishwa nje ya mkoa huo.
“Hapa wapo wabunge, madiwani na viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo, baadhi ya wabunge walipendekeza mkakati wa kutatua uzembe uliofanyika Mtwara, unapaswa kuchukuliwa kwa uangalifu usije ukasababisha madhara mengine kwa Chama na Serikali.
Walisema suala hilo halina budi kuchukuliwa kwa uangalifu hasa ikizingatiwa kuwa Chama cha CUF ndicho chenye nguvu mkoani humo ukilinganisha na vyama vingine vya upinzani.
Wabunge hao walikituhumu chama hicho kuwa kimekuwa kikijaribu kutumia vurugu hizo kama kigezo cha ushawishi wa kukubalika mkoani humo.