Monday, June 10, 2013

CHADEMA, CUF waunga mkono serikali taatu


Pro. Ibrahim Lipumba

Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti CUF Profesa Ibrahimu Lipumba kwa nyakati tofauti wameweka bayana kuwa wanaunga mkono Rasimu ya Katiba na hasa suala la Muungano wa Tanzania kuundwa na Serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mbowe Amesema mambo mengi yaliyopendekezwa na chama chake yamefanyiwa kazi na Tume ya Mabadiliko na kuishangaa CCM akidai kwamba inapinga rasimu hiyo hususan suala la Serikali tatu wakati kimsingi watu wa Tanzania Bara wamekuwa wakipunjika kwenye muundo wa sasa wa Muungano.
Akihutubia mkutano wa kampeni ya kuwania udiwani wa Kata ya Iyela katika Uwanja wa Bongonela, Mbeya jana jioni, Mbowe alisema chama chake kinataka kuona Serikali ya Tanganyika ikifufuliwa. Alikuwa akimnadi mgombea wa Chadema, Charles Mkela.
Alisema Chadema kinataka kuona Wazanzibari wakiwa na Serikali yao ili wajiamulie mambo yao na pia Watanganyika wawe na uongozi wao lakini waunganishwe na Serikali ya Muungano.
Alisema muundo wa sasa wa Muungano una matatizo. Kwa mfano, mbunge wa Zanzibar anawakilisha watu wachache zaidi ukilinganisha na mbunge wa Bara. Wananchi mtashangaa sote tunalipwa sawa.”
“Ila zikija Serikali tatu ina maana kuwa kila upande wa Muungano utatumia rasilimali zake. Haya mambo kulipana fedha nyingi kwa kazi kidogo yatakoma.”
Lipumba: Katiba ya Bara kwanza
Profesa Lipumba alisema hakuna mantiki ya kupiga kura ya maoni ya Katiba ya Muungano bila kuwa na Katiba ya Tanzania Bara na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Profesa Lipumba alisema mapendekezo ya msingi ya CUF ni kwamba, kura ya maoni isubiri kukamilishwa kwa rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar.
Alisema licha ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kufanya kazi nzuri ya kuratibu maoni bila kushinikizwa na matakwa ya CCM, kuna baadhi ya mambo ya msingi ambayo yameachwa kwenye rasimu.
“Huwezi kuacha vitu kama umilikaji wa ardhi, maliasili na rasilimali za nchi, elimu, afya na mazingira ya kukuza uchumi na uhuru wa Serikali za mitaa. Rasimu imeshughulikia mambo ya Muungano.”
“Maoni ambayo CUF tuliyatoa ikiwamo muundo wa Serikali tatu, kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, Rais kutangazwa baada ya kushinda kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zote, Spika kutokuwa mbunge na mengineyo yamepata nafasi.”
Source: Mwananchi

No comments: