Monday, July 29, 2013

Dk Slaa amwaga cheche kwenye Kongamano la Amani


Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Willibrod Slaa ameitupia lawama serikali ya Tanzania kuwa ndiye mchawi wa uvunjifu wa amani ya Tanzania.

Dk Slaa aliyasema hayo kwenye Mdahalo wa kujadili mstakabali wa amani ya taifa ulioandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mdahalo huo ambao kauli mbiu yake ilikuwa ni Mustakabali wa Amani na Usalama wa Wananchi wa Taifa Letu kwa Miaka 50 Ijayo, uliwashirikisha wanazuoni, wanasiasa, viongozi wa vyombo mbalimbali vya ulinzi na serikali.

Wachokoza mada walikuwa ni mhadhiri wa sheria wa chuo hicho, Dk. Onesmo Kyauke aliyegusia mfumo wa utendaji wa Jeshi la Polisi katika kusimamia amani ya nchi, Profesa Benadetha Kiliani, mtaalam wa sayansi ya siasa na utawala kwa umma na mwanahabari nguli na mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari, Dk. Ayoub Rioba.

Dr Slaa wakati akichangia mada alinukuu ripoti ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyomtuhumu aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, na Msajili wa Vyama vya Siasa ambapo alisema serikali imekuwa chanzo cha uvunjivu wa amani kwa kundamiza raia. 

Amesema amani sio suala la kuhubiriwa au kujadiliwa bali ni matokeo ya utekelezaji wa haki mbalimbali.

Dk Slaa pia alilalamikia vitendo vya ukatili vilivyofanywa Mtwara na vyombo vya dola dhidi ya wananchi, huku akimnyooshea kidole Brigedia Elia Athanas aliyekuwa amemwakilisha Mkuu wa Majeshi.

“Jeshi letu lilikuwa linaheshimika sana, lakini siku za hivi karibuni linaelekea kupoteza heshima yake kwa jamii, tukirejea mfano katika uchaguzi mkuu uliopita ambapo mnadhimu wa jeshi, Abdulrahman Shimbo, alivyotoa kauli yenye utata, jeshi linaingiaje kwenye siasa wakati suala la uchaguzi ni suala la kiraia?” alihoji.

Hoja ya Dk. Slaa kuhusu utendaji wa jeshi la wananchi mkoani Mtwara ilipingwa kwa haraka na Brigedia Athanas akisema: “Naomba kuweka wazi kuwa jeshi letu liko Mtwara, lina adabu na vitendo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa ni vya propaganda tu kama alivyosema Dk. Slaa.”
Licha ya kiongozi huyo kujitetea, mchangiaji aliyefuata, Julius Mtatiro ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Tanzania Bara), alithibitisha kuwa wanajeshi wanabaka na walitenda vitendo vya kikatili dhidi ya raia na viongozi wa chama hicho akiwemo mkurugenzi wao, Shaweji Mketo.
Mwakilishi wa NCCR Mageuzi, Faustine Sungura, alisema chama hicho hakiko tayari kufanya maandamano bali kinapambana kwa nguvu ya hoja na kwamba wataendelea kutumia nguvu ya hoja.

Naye mmoja wa wachokoza mada  Dk. Onesmo Kyauke aliliponda jeshi la polisi linavyokiuka sheria katika kutekeleza majukumu yake kiasi cha kuruhusu kuingiliwa na wanasiasa na kuelekezwa jambo la kufanya.

Bila kuuma maneno, mhadhiri huyo alimtaja wazi wazi Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), Mwigulu Nchemba, akidai kwa sasa analiendesha jeshi hilo kwa kuingilia majukumu ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mwendesha Mashataka Mkuu (DPP).

Alisema kuwa mwanasiasa huyo ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi, amekuwa akiwatuhumu wanasiasa wa vyama vya upinzani kuwa ni magaidi na polisi wamekuwa wakiwakamata na kuwafungulia mashtaka hayohayo anayosema kada huyo bila hata kuwa na ushahidi.

Dk. Kyauke alitolea mfano wa matukio ambayo Nchemba amekuwa akiyafanya kuwa ni pamoja na lile la kuonyesha ushiriki wa kupanga tukio la ugaidi la Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Wilfred Lwakatare.

Tukio lingine alisema ni wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani jijini Arusha, ambapo kiongozi huyo aliwataka wananchi wa jiji hilo kutochagua madiwani wa CHADEMA kwa kuwa ni chama cha ugaidi kwa madai kwamba ndio waliohusika kummwagia tindikali kijana wa CCM kule Igunga.

Kutokana na matamshi hayo, mhadhiri huyo alisema baadhi ya wanachama wa CHADEMA waliweza kukamatwa kama njia mojawapo ya kuisaidia polisi; jambo linalowafanya kama wasomi kujiuliza kuwa Mwigulu siku hizi kawa DCI au DDP?

Kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, alisema ndilo limekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa amani kwa kupoka haki ya Kikatiba ya wananchi kuandamana na kufanya mikutano huku akitolea mfano wa mauaji yaliyofanywa na jeshi hilo ya mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi, kijijini Nyororo, mkoani Iringa, wakati wa kuzindua matawi ya CHADEMA.

Katika mauaji hayo, alisema ushahidi wa wazi umeonyesha namna gani polisi walivyoshiriki na tume zote zilizoundwa zikamuelekezea kidole Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa na Msajili wa Vyama vya Siasa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa hadi leo zaidi ya polisi mwenye cheo kidogo akitolewa kafara huku mkubwa wake akiendelea kupandishwa cheo.

Pia alisema kumekuwepo na upendeleo wa jeshi hilo kwa kutetea chama tawala ikiwemo enzi za IGP Omar Mahita kudai kuwashikilia wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na majambia ingawa hadi leo wamekosa uthibitisho lakini kutokana na uongo huo wameshindwa kumchukulia hatua kiongozi huyo.

Katika mapendekezo yake, Kyauke aliitaka polisi kubadili mfumo wake wa kufanya kazi, na kuhoji kwa nini Tanzania ni dhambi kuandamana huku akimtaka Waziri Mkuu kufuta kauli yake ya kutaka wananchi kupigwa tu na jeshi hilo wanapokaidi amri.

Prof. Kilian kwa upande wake, alisema mpaka sasa bado kiini cha uvunjifu wa amani hakijagundulika na badala yake pande zote zimekuwa zikirushiana mpira ikiwemo serikali, wananchi na wanasiasa.

Alizitaja sababu zinazochangia matukio hayo kuwa ni pamoja na hali ya upinzani kuja juu hivyo chama tawala kinajihami kutokana na mabadiliko hayo, kuongezeka kwa kiwango cha umaskini na mfumo wa kiliberali ambao umechangia matabaka na uhuru wa kutoa maoni tofauti na enzi za ujamaa.

Naye Dk. Ayubu Rioba alisema suala la amani sio la kuombewa kanisani au msikitini bali ni la kisayansi zaidi na kudai kwamba wanasiasa wamekuwa wakijidanganya pale wanapowahimiza watu kuliombea taifa liwe na amani.

Rioba alikanusha vyombo vya habari kuwa vimekuwa vikichangia kuharibu amani na badala yake alivifananisha vyombo hivyo na bunduki ambapo kama isipotumiwa kamwe haiwezi kuharibu amani.

Akifafanua hili alisema vyombo vya habari vitaharibu amani endapo tu wanasiasa watavitumia na kuitaka jamii ielewe kwamba vyombo hivyo vina dhima kubwa kama mlinzi wa taifa na ndio maana wakati mwingine vinapendekezwa kuwa NGO’s ili viweze kufanya kazi kwa uhuru zaidi. 

No comments: