Wednesday, August 7, 2013

Tendwa ataka kuwa mshauri wa siasa, ampa ushauri Mutungi

John Tendwa
Msajili aliyemaliza muda wake John Tendwa amesema baada ya kustaafu ana mpango wa kufanya kazi za ushauri katika siasa za kimataifa na sio siasa za maji taka.
“Nahitaji muda kidogo kufikiri nitafanya nini ila napenda sana kuwa ‘international consultant’ kwenye masuala ya siasa, lakini pia ikumbukwe kwamba mimi ni mwanasheria ambaye nimekuwa katika masuala ya uwakili kwa takriban miaka 23. Muda utaongea nifanye nini, ngoja kwanza nikabidhi ofisi,” alisema Tendwa.
Tendwa alisema hawezi kumfundisha kazi Jaji Mutungi kwani anaamini atafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na taratibu kama ambavyo miongozo inavyotaka.
“Mutungi atafanya kazi kwa mujibu wa sheria, siku zote atafuata sheria na kutafsiri sheria maana yeye ni Jaji. Ninawaomba wadau wampatie ushirikiano maana sasa anakuja kufanya kazi na wanasiasa,” alisema Tendwa.
Alisema endapo Jaji Mutungi ataanza kubezwa na wanasiasa anatakiwa kujua ndani ya moyo wake kwamba anafanya kazi yake sawasawa.
“Ila kama ataona wanasiasa wanamsifia basi atakuwa kuna sehemu ambazo hatekelezi vyema majukumu yake. Kufanya kazi na wanasiasa kunahitaji busara na sio kufuata vitabu vya sheria vinasemaje,” alimshauri Jaji Mutungi.