Saturday, August 10, 2013

Rwanda yamjibu Kikwete kwa nidhamu, yachagua maneno ya kusema

Rais wa Rwanda Paul Kagame
Katika hali inayoonyesha serikali ya Rwanda sasa imeshtushwa na hotuba kali ya Rais Kikwete aliyoitoa hivi karibuni na kuzungumzia kauli za Rwanda za kumtukana, kwa mara ya kwanza serikali ya Rwanda imetoaa tamko linaloonyesha kuwa nchi hiyo imeanza kuwa na tahadhari katika kujibu masuala yanayomhusu Rais Kikwete.
Rwanda kupitia waziri wake wa Mambo ya Nuje, Louise Mushikiwabo, ilikaririwa ikieleza kwamba hawatajibu mapigo agizo la Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka Wanyarwanda wote waliolowea Magharibi mwa Tanzania kuondoka haraka.
Mushikiwabo alisema wako tayari kuwapokea na kuwalinda wote waliofukuzwa Tanzania kwa kisingizio kuwa ni wahamiaji haramu, akieleza kwamba anasikitishwa kwa kuwa Tanzania haikufanya jitihada yoyote kuwasiliana na Rwanda kuhusu suala hilo kabla ya kuchukua uamuzi huo.
“Ni uamuzi ambao umeshachukuliwa, hatukushirikishwa kwa namna yoyote na jukumu letu kama serikali na taifa ni kuwahakikishia ulinzi wote wanaokuja, na hili ndilo suala tunalolishughulikia kwa sasa,” alisema.
Kwa mujibu wa gazeti la New Times, Mushikiwabo aliwaeleza waandishi wa habari kwamba agizo hilo la Rais Kikwete pamoja na ushauri wa kuitaka Serikali ya Rwanda kuzungumza na wanamgambo hasimu wa FDLR waliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), hayatayumbisha uhusiano imara baina ya Watanzania na Wanyarwanda.
“Sisi si majirani tu, tuna mfungamano imara baina ya watu wetu pia, tuna mfungamano wa damu, wa kibiashara, na mengine mengi ya kutufanya tuendelee kuwa pamoja,” alisema na kutumia fursa hiyo kuwakaribisha Watanzania nchini Rwanda.
Watanzania wanaweza kuishi hapa kwa umri wowote wanaotaka. Tunawachukulia kuwa ni watu wetu muhimu kwenye fungamano la Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisisitiza.
Rais Kikwete wakati akihitimisha ziara yake mkoani Kagera alitoa agizo la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria na wahamiaji haramu ama kuondoka au kuhalalisha ukazi wao, huku akitoa wiki mbili kwa zoezi hilo kutekelezwa, kabla ya kuanza kwa operesheni ya kuwasaka watu hao.
Kauli hiyo ilitokana na kushamiri vitendo vya kihalifu katika eneo la Kanda ya Ziwa, Rais hakutaja jina la nchi ya wahamiaji hao. Kwa ukanda huo Tanzania inapakana na Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na DRC.
Pia, Rais Kikwete katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi alizungumzia kusikitishwa na kauli za shutuma, kejeli na udhalilishaji zilizotolewa na Rais Paul Kagame wa Rwanda dhidi yake.
Mvutano baina ya Rwanda na Tanzania ulianza kuwekwa hadharani Mei mwaka huu, baada ya Rais Kikwete kuishauri Rwanda kukaa na kuzungumza na FDLR wenye makao yao DRC, hatua ambayo haikuifurahisha Serikali ya Rwanda.
Wakati Rwanda ikieleza hayo jana Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue alizungumza na gazeti hili, na kutaka majibu ya kauli hiyo ya Rwanda yatolewe na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.