Saturday, November 17, 2012

Hali ya Sintofahamu Iringa: Mapadri wapigwa risasi Kanisani

MAPADRI wawili wa Kanisa Katoliki Parokia ya Isimani, Jimbo la Iringa, wamepigwa risasi na wamejeruhiwa vibaya na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa wa  Iringa, kutokana na watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuwavamia kwa silaha za jadi na bunduki, katika nyumba wanazoishi kwenye eneo la kanisa.

Paroko wa Kanisa hilo Angelo Burgio kutoka Italia (60) na msaidizi wake Herman Myala walikumbwa na mkasa huo usiku wa kuamkia jana.
Paroko wa Parokia ya Isimani, Baba Anjelo  Burgo  akiwa  kitandani  kwenye chumba maalumu katika Hosptali ya Mkoa wa Iringa wakti akisubiri kufanyiwa upasuaji kwa lengo la kutoa risasi zilizosalia mwilini baada ya  watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wakiwa na silaha za jadi na Bunduki kuvamia nyumba wanazoishi mapadri usiku wa kuamukia jana. Picha na Said  Ng’amilo 

Padri Burgio alijeruhiwa kwa kupigwa risasi mbili kifuani na kucharangwa mapanga, msaidizi wake Padri Myala alijeruhiwa kwa mapanga na kuburutwa chini kwenye ardhi.



Tukio hilo limetokea ikiwa ni siku moja tangu kuvamiwa kwa Kanisa Katoliki Jimbo la Iringa lililopo eneo la Kihesa mkoani humo, ambapo mlinzi wa kanisa hilo, Batholomea Nzigilwa (65) alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali kichwani.
Nzigilwa amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa, huku hali yake ikielezwa ikiwa ni mbaya.

Naye Padri Burgio alionekana akiwa amelazwa, huku akiwa ametundikiwa chupa ya maji  wakati akisubiri huduma ya upasuaji kwa  ajili ya kutolewa risasi mwilini.

Akizungumza kwa tabu, padri huyo alisema majambazi hao walifika eneo la Kanisa la Kihesa saa tano usiku wakiwa na  silaha mbalimbali za jadi na bunduki.

Alisema baada ya kumshambulia msaidizi wake, walimfyatulia yeye risasi kifuani wakati alipofungua mlango na kutaka kukimbia.

“Mimi baada ya kuwasikia nilifungua mlango kwa lengo la kutaka kukimbia ili nijinusuru, lakini hamadi wakanifyatulia risasi kifuani.

Nilianguka chini na walipoingia ndani walichukua fedha taslimu Sh3.5 milioni zilizokuwa chumbani kwangu na kisha kunikata na panga kichwani, ” alisema Burgio.  

Hata hivyo, padri huyo alisema, “Sisi tunawasamehe. Mimi na mwenzangu tumewasamehe tangu
walipofanikiwa kutushambulia na kukimbia. Tunawaombea msamaha kwa Mungu kwani yeye ndiye anayejua,” alisema Padri Burgio.

Source: Gazeti la Mwananchi