Baadhi ya ndugu na marafiki wa watuhumiwa wakikaguliwa |
MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), amemfutia kesi mmoja wa washtakiwa waliojumuishwa katika kesi inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake.
Pia katika kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, hakimu ameuamuru upande wa mashtaka uache utaratibu wa kumwingiza mahakamani mshtakiwa wa kwanza, Sheikh Ponda akiwa amefungwa pingu.
Aliyefutiwa mashtaka jana ni mshitakiwa wa 35 katika kesi hiyo, Rashid Omar.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka ndiye aliyetoa taarifa kuhusu uamuzi huo wa DPP wakati wa usikilizwaji wa maelezo ya awali wa kesi hiyo jana.
Kweka aliieleza mahakama kuwa, DPP kupitia kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya Omar.
Kutokana na uamuzi huo wa DPP, Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo aliamuru mshtakiwa huyo aachiwe huru.
Hata hivyo, wakati mshtakiwa huyo akiachiwa huru, Kiongozi wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Mukadamu Abdallah Swalehe aliunganishwa katika kesi hiyo.
Sheikh Swalehe alipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 2, 2012 na kusomewa mashtaka manne likiwemo la wizi wa mali ya Sh59.6 milioni, mashtaka ambayo yanahusiana na mashtaka ya Sheikh Ponda na wenzake waliopandishwa kizimbani kabla yake.
Hatua ya Sheikh Swalehe kuunganishwa na wenzake, ilisababisha upande wa Jamhuri ubadilishe hati ya mashtaka na kisha kusomwa upya.
Kwa mujibu wa hati hiyo mpya, washtakiwa wote 50 wanakabiliwa na mashtaka manne kwa pamoja, lakini Sheikh Ponda na Sheikh Swalehe walisomewa shtaka lingine zaidi na kufanya wawe na mashtaka matano.
Mashtaka yanayowakabili washtakiwa wote ni wizi, kula njama, kuingia kwa nguvu kwenye eneo lisilo mali yao kwa nia ya kutenda kosa na kujimilikisha ardhi kwa nguvu na kusababisha uvunjifu wa amani.
Shtaka la tano ambalo linawakabili Sheikh Ponda ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo na Sheikh Swalehe ambaye ni mshtakiwa watano ni la uchochezi.
Katika hatua nyingine, Hakimu Nongwa aliamuru Ponda asiingizwe mahakamani akiwa amefungwa pingu na badala yake aliitaka Jamhuri itafute utaratibu mwingine wa ulinzi, badala ya kutumia pingu hadi mahakamani.
Hatua ya Hakimu inatokana na maombi ya Wakili wa utetezi, Juma Nassoro aliyelalamikia utaratibu wa Ponda kuingizwa kwenye chumba cha mahakama akiwa amefungwa pingu mikononi.
Maelezo ya awali
Baada ya kusomewa mashtaka hayo upya, washtakiwa hao walisomewa maelezo ya awali ya mashtaka yanayowakabili.
Kweka alidai kuwa, Oktoba 12, 2012, washtakiwa hao walivamia kiwanja cha taasisi iitwayo Agritanza Ltd kilichopo Chang’ombe,Temeke jijini Dar es Salaam na waharibu msingi wa nyumba uliokuwa umeshajengwa.
Wakili Kweka alidai kuwa, washtakiwa walivamia kiwanja hicho kwa nguvu wakiongozwa na mshtakiwa wa kwanza (Ponda) na mshtakiwa wa tano (Swalehe) na kwamba, walikuwa wakikaa hapo hadi walipokamatwa Oktoba 16, mwaka huu.
Alieleza kuwa, Agritanza Ltd waliuziwa kiwanja hicho na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakatwa) ambayo ni taasisi iliyoundwa na kusajiliwa kisheria kutoa miongozo kwa Waislamu.
Alidai kuwa, chini ya wadhamini wake, Bakwata inamiliki mali mbalimbali zikiwemo majengo na viwanja, kikiwemo cha Chang’ombe Markazi, wilayaniTemeke, jijini Dar es Salaam.
Wakili Kweka aliendelea kudai kuwa, Juni 18, 2011 Bakwata kupitia bodi ya wadhamini wake iliingia makubaliano na Kampuni ya Agritanza Ltd kuuziana au kubadilishana kiwanja hicho.
Alidai kuwa, katika kuuziana kiwanja hicho, Bakwata walikubaliana na Agritanza walipe fedha pamoja na kuipa Bakwata kiwanja kingine kilichopo mkoani Pwani na kwamba, tangu siku hiyo umiliki wa kiwanja hicho ukahamishiwa kwa Agritanza.
Wakili wa utetezi
Hata hivyo washtakiwa hao, kupitia kwa wakili wao Nassoro waliyakubali majina yao na kuwepo kwa chombo kinachoitwa Bakwata, lakini wakakana kuwa chombo hicho ni kwa ajili ya Waislamu wote, wakidai kuwa ni kwa ajili ya baadhi ya Waislamu tu.
Kadhalika aliomba washtakiwa wapewe maelezo ya mlalamikaji, orodha ya mashahidi pamoja na vielelezo vitakavyotumiwa na upande wa mashtaka.
Akijibu hoja hizo, Kweka alidai kuwa kutoa orodha ya mashahidi wake pamoja na vielelezo si matakwa ya kisheria, hivyo Jamhuri haiwezi kulazimishwa.
Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 29, 2012 itakapoanza kusikilizwa mahakamani hapo. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo wako nje kwa dhamana isipokuwa Ponda na Swahele tu ambao dhamana yao imezuiliwa na DPP.
Source: Gazeti la Mwananchi
No comments:
Post a Comment