Wednesday, December 1, 2010

Hali bado ngumu Ivory Coast baada uchaguzi



Wafuasi wa upizani wanasema Rais Gbagbo hataki kuondoka mamlakani
Vurugu zimetokea katika makao makuu ya tume ya uchaguzi nchini Ivory Coast, baada ya wafuasi wa Rais Laurent Gbabgo kupinga kutangazwa kwa matokeo ya duru ya pili ya uchaguzi.

Mfuasi sugu wa Rais Gbabgo ambaye pia anahudumu kwenye tume ya uchaguzi, alizua utata pale alipochana karatasi iliokuwa na matokeo ya awali, akidai kuwa hayakuwa sahihi.

Vurugu hizo zimetokea huku wasiwasi ukitanda mjini Abidjan, siku ya tatu baada ya duru ya pili ya uchaguzi kufanyika.

Rais Gbabgo anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa aliyekuwa Waziri mkuu Alassane Ouattara.

Wafuasi wa Bw Ouattara wanadai kuwa Rais Gbabgo anataka kulazimisha utawala wake kwa kuzuia kutangazwa kwa matokeo hayo na wanaamini kuwa wameshinda uchaguzi huo.

Uchaguzi huo umelenga kuunganisha nchi hiyo iliogawanyika kwa pande mbili, kusini na kaskazini baada ya vita kutokea mwaka wa 2002.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hilary Clinton, amewataka viongozi hao waheshimu matokeo ya uchaguzi na walinde amani kwenye nchi ambayo inazalisha zao kubwa zaidi la kakao duniani. (BBC Swahili)

No comments: