Wednesday, December 1, 2010

Issa Hayatou akanusha madai ya rushwa




Afisa mkuu wa mchezo wa soka Issa Hayatou amekanusha vikali madai alihusika na ufisadi kwenye kipindi kilichorushwa na BBC cha Panorama.

Hayatou ambaye ni Makamu Rais wa shirikisho la FIFA amesema anatafakari kuichukulia BBC hatua za kisheria.

Kwenye kipindi cha PANORAMA kilichopeperushwa hewani siku ya Jumatatu, inadaiwa Hayatou alichukua hongo ya pesa za Kifaransa 100,000 sawa na paundi za Uingereza 12,900 mwaka wa 1995, kutoka kwa kampuni moja ya Uswizi ili kampuni hiyo ipewe mkataba mnono wa matangazo na FIFA.

Bwana Hayatou amesema pesa hizo zilikuwa zinatumika kufadhili Shirikisho la soka barani Afrika Caf.


" Pesa hizi hazikuwa zangu ila zilikuwa zitumike kwa maadhimisho ya miaka arobaini ya shirikisho la soka barani Afrika Caf.'' Alisema raia huyo wa Cameroon ambaye pia anaiongoza Caf.

"Wakati huo ISL ndio waliokuwa wafadhili wa Caf na walitoa pesa hizo kwa shirikisho hilo wala sio kwangu na kamati kuu ya Caf ilikubali na kuidhinisha''

''Nitakutana na mawakili wangu. Nitazungumza nao kisha nione hatua za kuchukua.''

Kipindi hicho cha Panorama kilimshutumu Bwana Hayatou kwa kuhusika kwenye ufisadi pamoja na viongozi wengine wa FIFA, Nicolas Leoz wa Paraguay na Ricardo Teixeira kutoka Brazil.

Viongozi hao watatu wamo kwenye jopo litakaloamua ni nani atakayekuwa mwenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2018 na 2022.

Kamati ya Kimataifa inayosimamia ya Olimpiki ilisema itafanya uchunguzi wake kuhusiana na madai hayo ya ufisadi kwa kuwa bw Hayatou ni mwanachama wa kamati hiyo.

Kundi lilalotetea Uingereza kupata nafasi ya kuwa wenyeji wa mashindano ya Kombe la Dunia wameishutumu BBC kwa kutoa ripoti hiyo ikiwa imesalia siku mbili tu kuamua nani atakuwa mwenyeji wa mashindano hayo. (BBC Swahili)

No comments: