Wednesday, January 18, 2012

Mauaji yazidi kutokea Sudan Kusini

 
Kundi la wapiganaji wa kikabila wenye silaha Sudan Kusini
Watu wenye silaha wamewaua takriban watu 51 wengi wakiwa wanawake na watoto katika mapigano ya hivi karibuni katika jimbo lenye mgogoro la Jonglei, gavana wa jimbo hilo Kuol Manyang amesema.
Waliojeruhiwa wamehamishiwa Juba makao makuu ya nchi.
Mfululizo wa mashambulizi ya kikabila kati ya makundi katika eneo hilo yamefanya maelfu ya watu kukosa makazi.
"Tunatarajia wengi wakiwa wamejeruhiwa kwa sababu walikimbia vijiji vyao usiku wa jana," Bw Manyang alisema.
Maafisa wameliambia shirika la habari la AFP kuwa mauaji hayo yalifanywa na kundi la Murle kwa kabila la Wadinka, kulipa kisasi kwa uvamizi mbaya wa mwezi uliopita katika mji wa Pibor.
Inafahamika kuwa baadhi ya Wadinka waliwasaidia wapiganaji wa Lou Nuer 6,000 ambao walishambulia Pibor.
Mzunguko wa ghasia hizi umedumu kwa miezi na mamia wameuawa. Zilianza kama wizi wa ng’ombe lakini zimesambaa na kushindwa kudhibitiwa.
Mwandishi wa BBC Afrika Mashariki Will Ross anasema mashambulio hayo yanaongezeka kuwa makali na si serikali wala askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa inavyoonekana wanaoweza kuwadhibiti.
Maafisa wanasema kuwa Jonglei ina ukubwa wa nchi ya Bangladesh na kwamba si rahisi kulinda kila kijiji.
Baadhi ya askari waliopelekwa katika eneo hilo wako Murle na eneo la kuzunguka Pibor lakini mashambulizi ya kisasi yanatokea katika jumuiya za Dinka na Lou Nuer.
Sudan Kusini, iliyopata uhuru wake mwaka jana imetangaza Jonglei kama ‘janga’ wakati UN imezindua harakati za dharura kusaidia walioathiriwa na mapigano hayo

No comments: