Friday, July 6, 2012

Mbowe aishupalia serikali kuhusu Dk Ulimboka

Freeman Mbowe aliyesimama na mwenye miwani akiwa ndani ya Bunge la Tanzania


Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ameitaka Serikali kuifanyia kazi Sheria ya Uchunguzi wa vifo vyenye utata kama ilivyoahidiwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika kikao cha bajeti mwaka jana.

Akizungumza katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu, Mbowe alisema kutotimizwa kwa ahadi hiyo kunaleta hisia kwamba Serikali inahusika katika baadhi ya vifo hivyo.Mbowe alisema kuwapo kwa vifo vya aina hiyo nchini huku baadhi yake vikihusishwa na vyombo vya dola, kunahitaji uchunguzi wa kina na yakinifu utakaofanywa na chombo huru ili kubaini wahusika na kisha kuwachukulia hatua za kisheria.

“Katika hotuba yako Waziri Mkuu ulikiri kuwepo kwa tatizo hilo na ulisema sheria ya  uchunguzi wa vifo vyenye utata itafanyiwa kazi na vifo vyenye utata vitafanyiwa uchunguzi, pengine unaweza kutwambia ni upi utekelezaji wa ahadi yao hiyo?” alisema Mbowe wakati anamwuliza swali Waziri Mkuu.

Mbowe alisema hisia za dola kuhusika katika mauaji na mateso  haya ya raia zimekuwa zikikuwa kila kukicha na hivyo taifa limepata sifa mbaya katika anga za kimataifa hasa baada ya kipigo cha Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka na wabunge wa Chadema jijini Mwanza.
Akijibu swali hilo Waziri Pinda alisema si kweli kuwa taifa linapata sifa mbaya kutokana na tukio la kupigwa kwa Dk Ulimboka.

“Sikubaliani na hoja kuwa sifa ya nchi imeharibika. Kwa lipi? Ukisema hivyo uwe na ushahidi wa hilo. Vilevile ukitumia mfano wa Ulimboka si mzuri. Jambo hili linahitaji kupatikana ukweli kwanza. Sasa tumeagiza uchunguzi wa kina na wa haraka kufanyike ili tupate ukweli huo,” alisema Pinda.

Kuhusu sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata, Waziri Mkuu Pinda alisema ni kweli aliahidi kwamba sheria inahitaji kufanyiwa marekebisho na kwamba tayari vyombo husika vimepewa maelezo ili kuwezesha mabadiliko hayo kufanyika.

“Wakati mwingine ni uzembe na ufuatiliaji duni. Si kweli kuwa Serikali inahusika. Sisi (Serikali) tutaendelea kufuatilia jambo hilo kwa umakini na kuhakikisha sheria hiyo inaanza kufanya kazi,” alisema  Pinda.

Habari hii imeandaliwa na Ibrahim Yamola, Fredy Azzah, Florence Majani, Dodoma

No comments: