Saturday, February 9, 2013

CHADEMA kuandamana kumpinga Spika Makinda na Naibu wakeKitendo cha kuzitupa hoja zilizowasilishwa bungeni na wabunge John Mnyika wa Chadema na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, kimesababisha chama kikuu cha upinzani Chadema, kuamua kufanya maandamano nchi nzima ili kuwashtaki kwa wananchi Spika wa Bunge, Anne Makinda  na Naibu wake Job Ndugai.

Maandamano hayo yatatanguliwa na mkutano wa hadhara utakaofanyika kesho Viwanja vya Temeke Mwisho, Dar es Salaam, sanjari na kuwapokea wabunge wake wanaorejea kutoka kwenye mkutano wa Bunge uliomalizika jana Dododma.


Chadema kimedai kuwa kanuni za bunge zina upungufu na kwamba kitendo cha spika na naibu wake kuzima hoja za wabunge hao kinadhihirisha kuwa viongozi hao wa mhimili huo wa taifa wameshindwa kulinda hoja zenye maslahi kwa wananchi na wameligeuza bunge kuwa ‘kijiwe cha CCM’.


Hoja zilivyozimwaWiki hii, katika kikao hicho cha Bunge, Mnyika aliwasilisha hoja binafsi akilitaka Bunge liazimie kuitaka Serikali ichukue hatua za haraka kuboresha upatikanaji wa majisafi na ushughulikiaji wa majitaka katika Jiji la Dar es Salaam.


Hata hivyo, hoja hiyo ilizimwa na Ndugai, ambaye baadaye aliruhusu kujadiliwa kwa hoja ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, hatua ambayo iliwafanya wabunge wote wa upinzani  kusimama kwa pamoja na kuanza kupiga kelele za kupinga hatua hiyo ya  Ndugai wakidai kwamba Naibu Spika huyo amevunja kanuni alizopaswa kuzisimamia.


Kitendo hicho pia kilisababisha kikao kuahirishwa kabla ya muda uliopangwa, huku hoja ya Profesa Maghembe  ya kupendekeza kuondolewa bungeni kwa hoja ya Mnyika ikiungwa mkono na wabunge wa CCM. 


Sambamba na tukio hilo Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia aliwasilisha hoja binafsi akidai Serikali haina mitalaa ya elimu na kutaka Bunge  kuunda kamati teule kuchunguza udhaifu huo.


Hata hivyo, hoja hiyo ilitupiliwa mbali, badala yake Ndugai aliunda kamati kuichunguza mitalaa hiyo kuangalia uhalali wake, kabla ya kuthibitishwa na Bunge.


Licha ya kuwa  Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa kuwasilisha bungeni mitalaa hiyo juzi, ambapo Mbatia alisema hakubaliani na mitalaa hiyo kwa maelezo kuwa kilichowasilishwa siyo kilichoahidiwa awali na Dk Kawambwa.

Tamko la ChademaKatika tamko la jana la Chadema mbele ya waandishi wa habari jana, Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira alisema :“Kwanza tutawapokea wabunge wote wa upinzani pale Ubungo na baadaye yataanza maandamano kuanzia eneo la Tazara, hadi katika Viwanja vya Temeke Mwisho, ambako utafanyika mkutano mkubwa wa hadhara.”


Akizungumzia kibali cha Jeshi la Polisi, Kigaira alisema tayari wameshatoa taarifa, uwanja wanaotarajia kufanya mkutano huo siku ya Jumapili hautakuwa na shughuli nyingine, hivyo hakuna kisingizio chochote wala sababu za kuzuiliwa kwa mkutano na maandamano hayo.


Alisema kilichofanywa na viongozi hao wakuu wa Bunge,  huku Serikali ikiwataka wananchi kuamini kuwa wabunge wa Chadema ni wakorofi ni sawa na ‘’kubaka demokrasia na ubabe wa kiti cha Spika.’’

Source: Mwananchi

No comments: