Thursday, October 11, 2012

Marekani kusaidia vita dhidi ya Ujangili Tanzania




Waziri wa Maliasili na Utalii wa Tanzania Khamis Kagasheki akizungumza Mkurugenzi Maliasili na Samaki wa Marekani Dan Ashe
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Marekani David Hayes amesema kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika mapambano dhidi ya ujangili nchini. Naibu Waziri huyo alisema hayo jana alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki jijini Washington DC.

“Wizara yangu ambayo inahusika na suala la uhifadhi katika maeneo yaliyotengwa kisheria itatoa ushirikiano wa karibu kwa Tanzania ili kuhakikisha kuwa vitendo vya ujangili katika maeneo ya ndani na nje ya hifadhi vinakwisha” alisema Bw. Hayes. 


Alisema kuwa maliasili nyingi duniani hasa baadhi ya wanyama kama tembo na faru wako katika hatari ya kutoweka kabisa kama jitihada za makusudi hazitafanywa na wadau mbalimbali ili kupiga vita ujangili.

 Aliongeza kuwa nchi yake itatoa msaada wa hali na mali kama vile kuunga mkono Tanzania katika mikutano mbalimbali inayojadili namna ya kudhibiti wimbi la ujangili hasa kutokana na kufanywa na mitandao mikubwa ya kimataifa yenye nguvu kubwa kifedha ambayo kwa kiasi kikubwa imechangia ongezeko la vitendo vya ujangili katika maeneo ya hifadhi.

Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki alimweleza mweyeji wake kuwa Serikali ya Tanzania imeshafanya juhudi mbalimbali za kupambana na ujangili kama vile kutoa adhabu kali kwa wale wote wanaopatikana na tuhuma za kujihusisha na ujangili ikiwemo watumishi wa serikali; kuendesha doria maalum katika maeneo ya ndani na nje ya hifadhi pamoja na kuendesha mafunzo ya kisasa na vifaa ambapo serikali kwa sasa ipo mbioni kununua helikopta itakayotumika kwa ajili ya shughuli za kudhibiti ujangili nchini.

Hata hivyo Waziri Kagasheki alikiri kuwa kazi hiyo bado ni kubwa na inahitaji ushirikiano wa karibu na Mataifa makubwa kama Marekani hasa kwa kuwa ujangili mkubwa unaofanyika unahusisha mitandao yenye nguvu kubwa ya kifedha pamoja na silaha kubwa za kivita na hivyo kuleta ushawishi mkubwa juu ya kuendelea kwa vitendo vya ujangili nchini.

Aliiomba Marekani kushirikiana kwa karibu na Tanzania ili kuweka mikakati ya pamoja ya kimataifa ya kupambana na tatizo hili pamoja na kutoa misaada ya kitaalamu itakayosaidia kupambana na tishio la kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai muhimu ulimwenguni jambo ambalo kizazi cha sasa kisipochukua juhudi za makusudi litaweza kuulizwa na vizazi vijavyo.

Katika hatua nyingine inayotia matumaini juu ya ushirikiano huu, mataifa haya mawili yalikubaliana kuwa Makubaliano ya Pamoja juu ya maeneo ya kushirikiana na namna bora ya uutekelezaji wa ushirikiano huu ambapo Makubaliano haya ya pamoja yanatarajiwa kuwekwa saini mwezi wa Disemba mwaka huu nchini Tanzania. 

Makubaliano haya ya pamoja ndiyo yatakuwa mahali pa kuanzia katika suala zima la namna ya kuendeleza ushirkiano wa pamoja baina ya nchi hizi mbili katika eneo la vita dhidi ya ujangili nchini.

Waziri Kagasheki na ujumbe wake walipata pia fursa ya kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusiana na masuala ya uhifadhi kama vile United States Fish and Wildlife Service; Council on Environmental Quality from the Department of Environment; National Fish and Wildlife Foundation na United States Senate Committee on Appropriations ambapo vita dhidi ya ujangili ilikuwa ajenda kuu ya mikutano hiyo.



No comments: