Thursday, October 11, 2012

Ripoti ya Mwandishi aliyeuawa yapingwa

Picha inayoonyesha polisi wakimpiga Daud Mwangosi kabla ya kifo chake

Marehemu Daud Mwangosi
 BAADHI ya wananchi, wakiwamo wasomi, wanasiasa na wanaharakati mbalimbali, wamekosoa ripoti ya Serikali kuhusu mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa Channel Ten mkoani Iringa, Daud Mwangosi linaripoti Gazeti la Mtanzania la Tanzania.

Ripoti hiyo imepingwa sambamba na ile ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), wakisema kuwa ripoti hizo hazijatoa majibu kuhusiana na kifo hicho na kwamba hayo ni matumizi mabaya ya fedha.

Maoni hayo yamekuja siku moja baada ya ripoti mbili za uchunguzi wa kifo cha mwandishi huyo kutangazwa hadharani jijini Dar es Salaam.Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa ripoti ya Serikali imeonyesha udhaifu mkubwa na kwamba imedhihirika wazi namna inavyoficha ukweli.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Azaveli Lwaitama, alisema ripoti zote mbili zimewahadaa wananchi na kwamba huko ni sawa na kuwadharau Watanzania.

“Ni dhahiri kuwa ripoti ile haikuwa na jambo lolote la maana, kwa sababu kitendo cha kudai kuwa polisi hawakushiriki katika mauaji wa Mwangosi, ni uongo ambao hauwezi kuaminiwa na Watanzania.

“Ni ripoti ambayo imeficha ukweli kwa Watanzania wakati picha za tukio hilo zipo na zinaeleza wazi namna polisi walivyohusika,” alisema.

Dk. Lwaitama alisema ni bora Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, angeitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake kuliko kutoa kitu alichokiita ripoti.

Kuhusu ripoti ya Baraza la Habari Tanzania (MCT), Dk. Lwaitama alisema ripoti hiyo haikuwa na tofauti kwa sababu mambo mengi yaliyobainishwa katika ripoti hiyo tayari yanajulikana kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bisimba, alisema kituo hicho kimeshangazwa na ripoti hizo, hususan ile ya Serikali.

“Ingawa hatujaipitia vizuri, bado tunaendelea na uchunguzi, lakini kikubwa tumeshangazwa sana na baadhi ya nukuu za ripoti ya Nchimbi kuwa polisi hawakuhusika na tukio hilo.

“Kwa sababu hili ni tukio la wazi, kuna ushahidi wa picha ambao unadhihirisha wazi namna polisi walivyohusika.

“Ripoti ya MCT ni nzuri, tunaiunga mkono kwa sababu imeeleza ukweli, hakuna kitu kilichopindishwa ingawa hakuna kitu kipya vilevile katika ripoti hiyo.

“Lakini kwa kuwa tunaendelea na uchunguzi wa ripoti hizo, Ijumaa wiki hii tunatarajia kutoa tamko letu kuhusu ripoti hizo mbili,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema matukio ya umwagaji damu kama yaliyotokea kwa Mwangosi yanatokana na chuki za kisiasa ambazo chanzo chake kikuu ni mapungufu katika sheria namba tano ya vyama vya siasa.

Alisema licha ya upungufu huo, Tume ya Uchaguzi (NEC) nayo inabidi kupewa uhuru wa kujitegemea katika kutekeleza majukumu yake.

“Kwa kweli ripoti zote sijazipitia, lakini kuna umuhimu wa kufanyia jambo hili utafiti ili kupata njia sahihi itakayosaidia kuondokana na tatizo la umwagaji damu.

“Kuendelea kwa utamaduni huo kutaliingiza taifa katika hali mbaya zaidi na hivyo, tumeamua kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutafuta njia sahihi yenye kuliweka taifa katika mfumo mzuri.

“Tumekubaliana kukutana kila baada ya miezi mitatu.....kikubwa ni kuhakikisha amani ya taifa inaendelea kudumishwa,” alisema.

Katika hatua nyinginemwananchi wa kawaida aliyejitambulisha kwa jina la Juma Khalfan,  aliiponda ripoti iliyotolewa na Serikali.

“Hiyo haikuwa ripoti ila ni taarifa tu...ambayo imejaa uhuni na dharau kwa wananchi, wasijitetee kuwa jambo hilo lipo mahakamani. Kama walikuwa wanajua lipo mahakamani kulikuwa na umuhimu gani wa kuendelea na uchunguzi?” alihoji.

No comments: