Monday, November 19, 2012

Mangula awapa Mafisadi CCM miezi 6 Wafungashe Virago



Makamu  Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tanzania Bara, Philip Mangula, amerejea na gia mpya katika uongozi wa chama hicho huku akiahidi atawang’oa viongozi walioingia katika uongozi wa kwa njia za mkato.

Mangula, ambaye aliondoka katika nafasi ya Ukatibu Mkuu mwaka 2007 baada ya kuishika kwa miaka 10, alisema jana kuwa  hana kundi lolote analoliunga mkono ndani ya Chama hicho hivyo atahakikisha viongozi wote waliopata madaraka kwa njia za hovyo hovyo katika uchaguzi uliomalizika hivi karibuni, wanang’olewa na kubakiza waliopata nafasi hizo kwa njia za halali.


Amesema baadhi ya wanachama wa CCM katika uchaguzi wa chama hicho uliohitimishwa wiki iliyopita, walinunuliwa kama sambusa na watu wachache wenye fedha ili wapange safu zao na kwamba ndani ya miezi sita, kila kitu kitajulikana na atafanya hivyo bila kumuonea mtu wala kumuogopa.

“Mimi nilikuwa nalima nyanya na mapalachichi huko kijijini kabla ya kuombwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ili kukisaidia Chama hiki kukitoa hapa kilipo kwa kuwa rushwa imekithiri ndani yake na kazi hii nitaifanya na kuikamilisha ndani ya miezi sita kuanzia sasa,” alisema katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa lengo la kuwapongeza viongozi wapya wa juu wa chama hicho.

“Malalamiko yapo kwa ngazi mbalimbali za Chama, nimeyakuta mezani kwangu, ndani ya miezi sita itajulikana na walioingia kihalali wataendelea, walioingia hovyo hovyo watatupwa nje,” alisema.

“Viongozi wameingia kwa rushwa na hii nimeipenda na nitaifanyia kazi vizuri sana bila ya kumuonea mtu na kumuogopa mtu yeyote ndani ya Chama chetu ili kurudisha heshima yake,” alisema.

Pamoja na Mangula kuahidi kupambana na rushwa, safu iliyomaliza muda wake akiwamo aliyekuwa Katibu Mkuu, Wilson Mukama na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Pius Msekwa, waliahidi kuwa wangewawajibisha makada wenye tuhuma za rushwa kupitia dhana ya kujivua gamba, lakini walishindwa.

Akihutubia mamia ya wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano huo,  Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alikiri kwamba chama hicho kwa sasa kimepoteza mvuto na kina taswira mbaya kwa jamii.

Rais Kikwete alisema njia pekee ya kurudisha heshima ndani ya CCM, ni kutafuta majawabu ya matatizo yaliyokifanya chama hicho kiwe na taswira mbaya na huo ndiyo ukweli.

“Mkigundua chama cha siasa hakiungwi mkono na watu wengi kama ilivyo sasa, lazima tujiulize na kutafuta majawabu hali hiyo imetokana na nini ili kupata fursa ya kujirekebisha na kukijenga,” alisema.

“Kuna watu hawataki kukubali ukweli huu kwamba CCM kimepoteza mvuto kama kilivyokuwa zamani, lakini huu ndiyo ukweli na kazi iliyo mbele yetu ni kukijenga kupitia mradi maalum ambao umeanzishwa na Chama hiki kwa sasa,” aliongeza Rais Kikwete.

Alisema kazi ya kukisafisha Chama itafanyika kwa muda wa miezi mitano kuanzia sasa na mageuzi ya kukibadili yameainishwa vizuri kinachotakiwa ni utekelezaji madhubuti.

Alikitaka chama hicho kufanya mikutano ya hadhara mara kwa mara ili kuzungumza na wananchi kama wanavyofanya wenzao wa upinzani badala ya kuacha wananchi waendelee kuwa na maswali mengi bila ya kupata majibu ya matatizo yao.

“Vyama vya siasa kazi yao ni kutupiga madongo sasa kama tutakaa kimya muda wote hatuwezi kupona, viongozi wa CCM mna mashangingi kwa nini msiyatumie kwenda kwa wananchi?” Alihoji Rais Kikwete.

Alisisitiza kwamba kazi ya kukijenga chama hivi sasa ni `mwendo mdundo na nginja ngija' lengo lake kubwa likiwa ni kukijenga Chama na kurudisha heshima.



Kuhusu uteuzi wa wajumbe wa Kamati Kuu (CC), Rais Kikwete alisema kazi hiyo itafanyika Januari, mwakani.

Alifafanua kuwa Chama kimetoa muda huo ili kuangalia wasifu wa kila mjumbe anayestahili kupata nafasi hiyo.

Awali akimkaribisha Mangula katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama hicho, Abdulrahman Kinana, alisema kuna kundi la wanachama wachache wananunua uongozi ili kupanga safu zao na kwamba muda wa kuwatimua umefika.

No comments: