Monday, November 19, 2012

Tanzania,Malawi Wingu Zito: Mazungumzo yakwama tena

Rais Mstaafu wa Msumbiji Joachim Chissano huenda akawa Msuluhishi wa mgogoro wa  mpaka wa ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi

BAADA ya mvutano wa muda mrefu hatimaye Serikali  za Tanzania na Malawi zimekubaliana kupeleka mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa katika jopo la viongozi wastaafu  wanaoshughulikia migogoro ya nchi mbalimbali barani Afrika.

Hatua hiyo imekuja baada ya pande hizo mbili kushindwa kuafikiana katika mazungumzo yaliyomalizika jana jijini Dar es Salaam, yaliyowakutanisha mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo mbili sambamba na viongozi mbalimbali wa serikali za nchi hizo.



Uamuzi huo umekuja siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe kuwaeleza waandishi wa habari kwamba Ziwa Nyasa ni urithi wa nchi tatu Tanzania, Malawi na Msumbiji na hivyo siyo sahihi upande wowote kati ya nchi hizo kudai unamiliki sehemu kubwa ya ziwa.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mazungumzo hayo, Membe pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Muganda Chiume alisema viongozi hao wastaafu watasaidia kumaliza tatizo hilo.

Membe alisema mapendekezo ya mazungumzo hayo yatapelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Malawi, Joyce Banda, wao watapeleka barua katika jopo hilo.
“Mazungumzo yetu naweza kusema tumekubaliana na pia hatujakubaliana, hivyo tumeamua kwenda katika hatua nyingine ya usuluhishi ambayo ni kwa jopo la viongozi wastaafu  linaloongozwa na Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano,” alisema Membe na kuongeza:
“Nitapeleka barua hiyo Machi 24 mwakani na endapo jopo hili litashindwa kufikia mwafaka tutaangalia uwezekano wa kwenda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ).”

Membe alifafanua kuwa Serikali ya Tanzania inaweza kuipeleka Serikali ya Malawi ICJ, lakini Malawi haiwezi kuipeleka Tanzania katika mahakama hiyo kutokana na kuwa nchi hiyo haikusaini makubaliano ya lazima.

Kwa upande wake Chiume alisema kuwa uamuzi utakaotolewa na jopo hilo wataukubali kwa kuwa wanaliamini katika utendaji wake wa kazi.

Alisema kuwa Malawi ilifurahishwa na kauli ya Rais Kikwete wakati akizungumza katika mkutano mkuu wa CCM uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma kwamba, nchi hizo mbili hazitaingia vitani.
“Kikwete na Banda wote kwa pamoja wamekuwa wakitoa kauli nzuri ambazo zinaonyesha kuwa nchi hizi mbili hazitaingia vitani kitu ambacho ni kizuri,” alisema Chiume.

Mgogoro huo ulianza Julai mwaka huu baada ya Malawi kuanza kufanya utafiti wa mafuta katika eneo la Tanzania, hali ambayo ilisababisha serikali hizo mbili kuanza kulumbana.

Serikali ya Tanzania ilipiga marufuku ndege za utafiti wa mafuta za Malawi kuruka katika anga ya Tanzania.

Source: Gazeti la Mwananchi

No comments: