Friday, November 30, 2012

Tanzania ndani ya Ugomvi na Televisheni ya Marekani CNN

Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Tanzania Assah Mwambene

Serikali ya Tanzania imekitaka kituo cha televisheni cha Kimataifa cha CNN kusahihisha taarifa potofu ilizotoa kuhusu mgogoro wa mpaka unaoendelea kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.

Taarifa hizo zinaonyesha kwamba mpaka wa Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa upo kwenye ufukwe wa Pwani ya Tanzania jambo ambalo Serikali imesema siyo sahihi.

Akiongea na waaandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO) Assah Mwambene amesema Serikali ya Tanzania imesikitishwa sana na taarifa hiyo na kuitaka CNN kuisahihisha mara moja.

“Tumesikitishwa sana na taarifa hiyo na tunashangaa kuona chombo kikubwa kama CNN wanaweza kutoa taarifa za uongo kwa kiasi hicho” amesema Bw. Mwambene.

Amesema ukweli ni kwamba unapozungumia eneo la Tanzania kilometa za mraba 947,300 (947,300 sq km)  ikiwa ni pamoja na  nusu ya eneo la ziwa kaskazini mwa mpaka wa Tanzania na Msumbiji na kwamba mpaka upo katikati ya ziwa kama ilivyo kwa mpaka wa Malawi na Msumbiji.

Kwa muda wa siku tatu kuanzia tarehe 24 Novemba, 2012, CNN International yenye makao yake Makuu nchini Marekani  imekuwa ikiendesha  kipindi kuhusu mgogoro wa Tanzania na Malawi na kuonyesha kwamba mpaka uko pembezoni mwa ufukwe wa Tanzania.

Bw. Mwambene amesema kuwa suala hilo hivi sasa linatarajiwa kupelekwa katika Baraza la Marais wastaafu wa Nchi za Umoja wa SADC kwa ajili ya kulitafutia ufumbuzi.

Wakati huo huo, Sherehe za miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania bara zinatarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam Desemba 9 mwaka huu.

Kauli mbiu za sherehe za uhuru mwaka huu ni uwajibikaji , uadilifu na uzalendo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu.

IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI