Sunday, December 2, 2012

Sasa Kimewaka!!!! Vigogo walioficha Mabilioni Uswis hawana pa kutokea!!!

Mwanasheria Mkuu Jaji Frederick Warema
SERIKALI imeamua kuunda kikosikazi kitakachohusisha Idara ya Usalama wa Taifa,  Polisi wa Kimataifa (Interpol) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa ajili ya kuanza uchunguzi kuhusu  Watanzania wanaotuhumiwa kuficha kiasi cha Sh314 bilioni nchini Uswisi.

Hatua hiyo ya uchunguzi inatokana na Bunge kutoa maazimio ya kuitaka Serikali kufuatilia sakata hilo katika kikao chake kilichopita mjini Dodoma na kutoa majibu katika kikao cha Bunge cha Aprili mwakani.

 Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amatangaza hayo na kusema “Tuhuma hizo siyo jambo dogo na Serikali haiwezi kuzipuuza, sasa tunachukua hatua madhubuti.”
Jaji Werema alisema kuwa Serikali imeshapiga hatua katika kufanya uchunguzi huo.
“Tumepiga hatua katika suala hili, ila ukianza kusema sana utakuwa unaharibu. Tumeamua kuwa na kikosi maalumu cha upelelezi kitakachoshirikisha Idara ya Usalama wa Taifa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Wizara ya Fedha na wachunguzi binafsi wakiwamo Polisi wa Kimataifa (Interpol) pamoja na Benki ya Dunia (WB).
“Serikali inaweza kuwashirikisha watu wengine kama Benki ya Dunia (WB) na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kwa ajili ya kusaidia uchunguzi huo.”



Aliongeza kuwa katika timu hiyo, wameamua kumshirikisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kutaka ukweli wa sakata hilo.
“Tumeamua kulifuatilia jambo hili, kama tutafanikiwa litakuwa jambo jema. Kama hatutafanikiwa tutakuwa tumejaribu,” alisema.

Hata hivyo, Werema alisema kuwa, bado hawajamwita Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema kwa ajili ya ushauriano zaidi.
“Unajua kuwa mwanasheria mkuu siyo kujua kila kitu, Zitto pia anaweza akawa na mbinu, ambazo zitasaidia katika jambo hili,” alisema Werema.

Hivi karibuni akiwa jijini Mwanza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika alisema kuwa Serikali ya Uswisi imeitaka Tanzania kuwasilisha kwake majina ya watu wanaotuhumiwa kuficha mabilioni ya fedha nchini humo, kama sharti la kusaidia uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la Kiingereza nchini, maofisa wa Uswisi walitaka ushahidi zaidi wa majina kama sharti la kutoa ushirikiano katika uchunguzi huo.

Kwa mujibu wa habari hizo, maofisa hao waliwataka wenzao wa Tanzania kupeleka majina ya wahusika, pia kutoa ushahidi usio shaka unaoonyesha nani alimpa nani rushwa, kuonyesha mazingira ya rushwa yaliyosababisha kupatikana kwa fedha hizo.

Maofisa hao pia walitaka Serikali ya Tanzania kuonyesha jinsi fedha hizo zilivyohamishwa hadi kwenye benki zao.

Akizungumzia masharti hayo, Zitto alisema uchunguzi utakaofanywa utafuata mfumo wa uchunguzi binafsi na kubainisha kuwa, kufuata mfumo wa kiserikali kunaweza kuwa na vikwazo vingi.
“Sisi hatufuati mfumo wa kiserikali, mfumo wa kiserikali ndiyo una masharti hayo. Sisi tunafuata mfumo wa uchunguzi binafsi,” alisema Zitto.

Source: Mwananchi