Wednesday, January 23, 2013

Hali ya Afya ya DCI Manumba sasa inatia Matumaini


HALI ya afya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba aliyelazwa Hospitali ya Aga Khan imeanza kutia matumaini.

Manumba alilazwa katika hospitali hiyo tangu Januari 15, mwaka huu akisumbuliwa na malaria kali ambayo pia iliathiri viungo vyake vya mwili, hata hivyo jana hali yake ilielezwa kuwa imeanza kuridhisha.Taarifa fupi iliyotolewa na Hospitali ya Aga Khana kuelezea maendeleo ya afya ya Manumba, ilisema juhudi za utoaji matibabu zinaendelea na kwamba afya yake inaendelea kuridhisha.
“DCI Manumba bado anaendelea na matibabu na hali yake inaendelea kuwa ya kuridhisha. Taarifa za maendeleo ya ugonjwa wake itaendelea kutolewa kila siku hapa hospitalini,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, viongozi mbalimbali wa kitaifa wameendelea kufika kumjulia hali.
Jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Mwingi alifika hospitalini hapo na kupata maelezo kuhusiana na maendeleo ya afya ya Manumba.

Viongozi wengine ambao tayari wamefika hospitalini hapo, ni Rais Jakaya Kikwete na mke wake, Salma.

Pia, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye alitumia dakika 15 kumjulia hali na baadaye aliaga na kuondoka.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Naibu wake, Pereira Silima, Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, Mkuu wa Polisi, Said Mwema na maofisa wengine wa vyeo vya juu wa polisi.

Manumba amelazwa kwenye chumba cha Wagonjwa wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), baada ya afya kuimarika huenda akapelekwa nje.

No comments: