Tuesday, January 8, 2013

Maoni Katiba Mpya Moto: Vyama vyatema cheche

Wajumbe wa Tume ya Katiba wakisikiliza maoni ya Vyama vya siasa

Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini Tanzania, jana ilianza kukusanya maoni ya vyama vya siasa katika mchakato wa Katiba Mpya, huku baadhi ya vyama hivyo vikitoa mapendekezo mbalimbali kuhusu suala la urais.
Vyama vilivyozungumzia urais katika mkutano huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam ni CCM, CUF na Chadema.

Taarifa za vyama hivyo zilipatikana baada ya wawakilishi wao kuwasilisha maoni kwenye tume hiyo katika mkutano wa ndani ambao waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia.

Wakati CCM ikitaka Katiba ijayo iruhusu mgombea binafsi, Chadema imependekeza Mtanzania yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 aruhusiwe kupiga kura na kugombea nafasi yeyote ya uongozi nchini. CUF imependekeza Muungano wa Mkataba.Mwanasheria wa Chadema ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema chama hicho cha upinzani, kimependekeza Katiba Mpya imtambue mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuwa ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa kushika nafasi yoyote ya uongozi nchini.

“Haingii akilini kwa mtu mwenye umri wa miaka 18 anakubalika kupiga kura na kumchagua kiongozi anayemtaka, lakini yeye mwenyewe hakubaliki kugombea nafasi yoyote ya uongozi ikiwamo urais, ubunge na udiwani,” alisema Lissu.

Alihoji “Kama Katiba ya sasa inamtambua mtu mzima kuwa ni yule anayeanzia umri wa miaka 18, kwa nini linapokuja suala la kuchaguliwa kwa ngazi zote ananyimwa haki hiyo hata kama ana vigezo vingine?”
Pia Lissu alisema kuwa Katiba Mpya haina budi kuanzisha utawala wa majimbo yasiyozidi kumi ili kuleta uwiano katika matumizi ya rasilimali kwenye maeneo yote ya nchi.

Aliyataja majimbo hayo kuwa ni Jimbo la Nyanza Magharibi ambalo litajumuisha mikoa ya Kagera, Geita na Shinyanga; Nyanza Mashariki mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu, Ziwa Tanganyika kwa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa na Jimbo la Kati litakalojumuisha mikoa ya Dodoma, Tabora, Singida na Iringa.

Mengine na mikoa yake kwenye mabano ni Jimbo la Kaskazini ( Arusha, Manyara na Kilimanjaro), Pwani ya Kaskazini (Tanga, sehemu za Pwani na sehemu za Morogoro), Jimbo la Dar es Salaam, Jimbo la Pwani Kusini (Mtwara, Lindi, Wilaya za Mafia, Rufiji na Ulanga) na Kanda ya Nyanda za Juu (Njombe, Mbeya na Ruvuma).

Mwakilishi wa CCM, Andrew Chenge alipendekeza kuwapo kwa mgombea binafsi katika nafasi zote ili kutoa fursa ya wananchi wasio wanachama wa chama chochote cha siasa kupata nafasi ya uongozi.

Alisema, kitakachofanyika ni kitengeneza mazingira mazuri ambayo yatawezesha mgombea huyo kupatikana bila ya kuwapo kwa itikadi za udini au ukabila.

“Mapendekezo ya chama chetu ni kuwapo kwa mgombea binafsi ili kushiriki kwenye nafasi zote za uongozi. Hii itasaidia kuondoa ubaguzi au kuleta udini, jambo ambalo linaweza kutoa fursa kwa wananchi wasio na udini wala chama kushiriki kwenye nafasi ya uongozi,”alisema Chenge.

CUF Serikali tatu
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema kuwa, chama hicho, kimependekeza kuwa na mkataba katika masuala mbalimbali yanayohusu Muungano.

Alisema sera ya CUF ni kuwa na Serikali tatu; Serikali ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar.
“Tumependekeza kuwa na Serikali tatu ambazo zitasaidia kuondoa migogoro ya masuala ya Muungano kwa sababu kila mmoja itakuwa inajitegemea,” alisema Lipumba.

Aliongeza kuwa katika sera hiyo, itawezesha kuainisha mambo mbalimbali ambayo yataweza kuondoa migongano ya kimaslahi yatakayojitokeza.
Alisema kutokana na hali hiyo, migogoro ya Muungano inayojitokeza katika maeneo mbalimbali, itaweza kupatiwa ufumbuzi kwa wakati bila ya kuwepo kwa matatizo yoyote.

Profesa Lipumba alisema, mbali na suala hilo, CUF pia imependekeza kuwe na tume huru ya uchaguzi ambayo itafanya kazi bila ya kuegemea upande wowote.

Alisema kutokana na hali hiyo, tume hiyo itaweza kuwa na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali ikiwamo za siasa, asasi za kiraia, ofisi ya msajili, wawakilishi wa wanawake, wazee, na vijana, jambo ambalo litasaidia kupata matokeo ya haki.

“Kukiwa na uwakilishi kutoka taasisi mbalimbali, kutasaidia kufanyika kwa uchaguzi ulio huru na wa haki. Jambo hilo linaweza kupunguza migogoro inayojitokeza hasa wakati wa uchaguzi,” aliongeza.

Awali Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba alisema kuwa lengo la kufanya usiri kwenye mkutano huo ni kutoa fursa kwa makundi hayo kutoa maoni yao bila ya kuingiza itikadi za siasa.

“Tumewaita ili waweze kutoa maoni yao bila ya kuingiza uhalisia wa maoni yao na si mambo yao ya siasa. Hii itasaidia kupata maoni ya kweli ambayo hayafungamani na mambo ya kisiasa,”alisem Jaji Warioba.

Aliongeza, ikiwa wamemaliza kutoa maoni yao wanasiasa hao wanaweza kuzungumza na waandishi ili waweze kuwapa taarifa ya yaliyojiri ndani ya mkutano huo.

Source: Mwananchi

.

No comments: